Tuesday 11 April 2017

ROMA AVUNJA UKIMYA SAKATA LA KUTEKWA MBELE YA MWAKYEMBE

Mwanamuziki Roma Mkatoliiki alipozungumza na Waandishi wa Habari kuhusiana na sakata la kutekwa nyara.
Mwanamuziki Roma Mkatoliiki alipozungumza na Waandishi wa Habari kuhusiana na sakata la kutekwa nyara.
img-20161130-wa0008

Mwanamuziki Roma Mkatoliki hatimaye leo ametoa ya moyoni kufuatia yeye na wasanii wenzake 2 pamoja na mfanyakazi wa ndani kutekwa na kuteswa na watu wasiojulikana siku ya Jumatano wiki iliyopita katika Studio za Tongwe jijini Dar es salaam na kupatikana Jumamosi wiki iliyopita.

Akizungumza na Waandishi wa Habari kwenye ukumbi wa Idara ya Habari maelezo leo Roma amesema walikuja watu waliokuwa na silaha za moto, wakawaamuru kuingia kwenye gari na kisha wakafungwa vitambaa usoni na pingu mkononi na kupelekwa eneo ambalo hawajalijua hadi sasa.

Amesema baada ya kufikishwa katika eneo hilo waliteswa ikiwemo kupigwa pamoja na kuhojiwa kwa muda wa siku tatu mfululizo, hivyo kupata maumivu makali kwenye miili yao.

Roma amesema kuwa mpaka sasa hawana uhakika na usalama wao kwa kuwa mahali walipokuwa hapakuwa pazuri.

“Kama alifanyiwa daktari, baadaye akafanyiwa msanii, usishtuke kesho akafanyiwa mwandishi wa habari, au Mbunge.”Alisema Roma.

Hata hivyo Roma ameacha maswali mengi ikiwemo nini sababu ya kutekwa kwao na watu gani waliohusika na utekaji huo pamoja na kuwapa mateso makali.

Katika mitandao ya kijamii inadaiwa kuwa wimbo uliopelekea wasanii hao kutekwa ni ule unaoitwa ‘Tanzagiza’ulioimbwa na msanii Sifa Digital video yake ipo Youtube.

Aidha katika mkutano huo Roma aliambatana na Waziri Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dkt. Harrison Mwakyembe kama waziri mwenye dhamana ya Wasanii na kazi zao ambapo kwenye mkutano huo alisema alipata hofu kusikia Roma ametekwa na watu wasiojulikana hivyo amehudhuria ili afahamu nini kilitokea.

Baadhi ya watu kwenye mitandao ya kijamii wamedai kuwa Roma ameshindwa kuelezea ukweli wa kile kilichotokea kutokana na kuhofia usalama wake kwa sasa ikiwa ni miezi minne tangu msaidizi wa Freeman Mbowe Ben Saanane atekwe na haijulikani alipo hadi sasa.

clouds stream