Watu 100 wamekamatwa mjini Mombasa Pwani ya Kenya kufuatia mashambulizi yaliyofanywa ndani ya kanisa moja mjini humo siku ya Jumapili.
Watu waliokuwa wamejihami kwa bunduki na kufunika nyuso zao waliwapiga risasi waumini wa kanisa moja mtaani Likoni na kuwaua watu wanne.
Polisi wanasema kuwa watu watatu waliokuwa wamejihami walivamia kanisa la Joy Jesus na kuanza kuwafyatulia waumini risasi kiholelea.Watu wawili walifariki papo hapo wengine wakifariki hospitalini wakati wakipokea matibabu. Wengine 17 walijeruhiwa vibaya.
Kadhalika polisi walisema kuwa washukiwa wakuu wa shambulizi hilo wametoweka
Hakuna mtu yeyote aliyekiri kufanya mashambulizi hayo , ila Kenya imekuwa ikishuhudia ongezeko la mashambulizi tangu kuanza kujihusisha na vita nchini Somalia mwaka 2011.
Jeshi la Kenya linasaidiana na wanajeshi wa Muungano wa Afrika kupambana na kundi la wanamgambo la Al Shabaab.
Hali ya usalama imedhibitiwa mjini humo kufuatia shambulizi hilo ambalo limekuja siku chache tu baada ya polisi kunasa washukiwa watatu wa ugaidi wakiwa na mabomu mawili makubwa tayari kufanya shambulizi kubwa.
Pia walinasa vilipuzi vingine ndani ya gari lililokuwa limeegeshwa karibu na kituo cha polisi.
Mji wa Mombasa wenye sifa ya utalii, umekuwa ukikumbwa na suitofahamu ya kiusalama kutokana na vijana wengi kujiunga na itikadi kali za dini hiyo.