Polisi achunguzwa kwa kumtorosha na kumweka kinyumba mwanafunzi wa kidato cha tatu
Askari
huyo anatuhumiwa kumrubuni mwanafunzi huyo kuwa atamnunulia magauni
mawili, blauzi mbili, sketi mbili pamoja na kiasi cha Sh 100,000.
Pamoja
na kumtorosha mwanafunzi huyo ambaye jina lake limehifadhiwa, askari
huyo na mwanafunzi, walipata ajali ya pikipiki waliyokuwa wakisafiria
kutoka mjini Moshi kwenda Kibosho, Septemba 27 majira ya saa 9 alasiri
na kulazwa hospitali ya Kibosho.
Kaimu
Kamanda wa Polisi mkoani Kilimanjaro, Moita Koka alithibitisha kupata
taarifa za askari huyo na tuhuma dhidi yake na kuongeza kwamba maofisa
wake wameanza kuchunguza tukio hilo ili hatua za kisheria ziweze
kuchukuliwa pale itakapothibitika.
“Hata mimi nasikia taarifa hizo za askari kumtorosha mwanafunzi na kuwa na uhusiano wa kimapenzi, lakini hilo siwezi kulizungumzia maana halijathibitika, nimetuma maofisa wangu wachunguze wakinipa taarifa nitatoa,” alisema.
Aidha,
Kamanda Koka alisema taarifa alizonazo ni juu ya kupata ajali kwa
askari wake akiwa amembeba msichana, lakini hajapewa taarifa kama
msichana huyo ndiye mwanafunzi anayezungumziwa na kama kweli wana
mahusiano ya kimapenzi ama la.
“Kwa ujumla hili tukio hasa upande wa mapenzi siwezi kulizungumzia, ninachofahamu na ambacho nimekitolea maelekezo ni kutaka kupewa taarifa za ajali inayozungumziwa… lakini hili la mahusiano nalo nimetaka nipewa taarifa zake, ikibainika sheria itachukua mkondo wake,” alisema.
Kwa
upande wake, diwani wa kata ya Okaoni na mwenyekiti wa halmashauri ya
wilaya ya Moshi Vijijini, Moris Makoi, alithibitisha taarifa za askari
kumtorosha mwanafunzi huyo na kujihusisha na mahusiano ya kimapenzi.
Makoi
alisema askari na mwanafunzi huyo pia walipata ajali eneo la Memorial
barabara kuu ya Moshi/Arusha wakati wawili hao wakirejea kutoka Moshi
mjini walikokuwa wamejificha kurejea Kibosho.
Naye
mwanafunzi huyo, akiwa katika wodi namba tano hospitali ya Kibosho,
alikiri kupewa ahadi ya kununuliwa nguo na Sh 100,000 ambazo hakupewa.
Alisema,
baada ya kufika mjini Moshi alikwenda kununuliwa vitu hivyo na kwenda
nyumba ya kufikia wageni ambako walikuwa na mahusiano ya kimapenzi na
wakati wakirejea Kibosho wakiwa na pikipiki hiyo walipata ajali na
kukimbizwa Hospitali ya Rufaa ya KCMC.
“Wakati tunatoka mjini tulipata ajali na nilipoteza fahamu na majira ya usiku nilijikuta nimelazwa Hospitali ya KCMC na siku iliyofuata yule askari alikuja na kunichukua na kunirejesha nyumbani,” alisema.
Hata
hivyo, mwanafunzi huyo alisema baada ya kufika nyumbani maumivu
yaliendelea kuwa makali na kuamua kupelekwa katika hospitali ya Kibosho
kuendelea na matibabu.
Akizungumzia
tukio hilo, muuguzi wa zamu wa Hospitali ya Kibosho, Erin Mmassele
alikiri kumpokea mwanafunzi hayo na kuongeza kuwa anaendelea vizuri
licha ya kuwa na majeraha miguuni.