Wednesday, 9 August 2017

Ifahamu Simba SC Na Simba Day

Nembo ya Simba
Nembo ya Simba
IMG-20170426-WA0006
Klabu ya Simba ina majina mbalimbali ya utani kama vile ‘Wekundu wa Msimbazi’ na ‘Lunyasi’ na ina makao yake makuu katika mtaa wa Msimbazi jijini Dar es Salaam.
Timu hii ilianzishwa mwaka 1936 jijini Dar es Salaam ikitumia jina la Queens lakini baadaye lilibadilisha jina na kuitwa Eagle kabla ya kubadilishwa tena na kuitwa Sunderland –jina lililotumika hadi mwaka 1971 ambapo ndipo jina la Simba Sports Club lilianza kutumika.
Ingawa tayari jina la Sunderland lilikuwa maarufu na kubwa tayari, lilibadilishwa na kuwa Simba; jina la mfalme wa msituni, ikiwa ni kutokana na pendekezo la aliyekuwa Rais wa Zanzibar, Hayati Sheikh Abeid Amani Karume, ambaye alishauri jina libadilishwe wakati akiweka jiwe la msingi la ujenzi wa jengo la makao makuu ya klabu mtaa wa Msimbazi.
Katika majina yaliyopendekezwa, jina la Simba lilikubaliwa zaidi na wengi na likaamuliwa kutumika kuanzia mwaka huo wa 1971. Simba ilianza kutanuka zaidi wakati ikitumia jina la Sunderland.
Ilikuwa na matawi yake katika maeneo mbalimbali jijini Dar es Salaam ambapo ziliundwa timu zilizokuwa na kazi ya kupika wachezaji waliokuja kuchezea Simba baadaye. Miongoni mwa timu hizo ni Morning Stars, Canada Dry, Liverpool na Ilala Stuff, ambako huko mchezaji aliyeonekana kukomaa alipelekwa kukipiga Sunderland.
Klabu hiyo iliona ni vema ikaanzisha siku ya kuwakutanisha mashabiki wake kabla msimu mpya wa ligi haujaanza ili kuweza kufanya mambo mbalimbali ikiwamo kutambulisha jezi, wachezaji wao.
Ndipo kile kinachofahamika kwa sasa kama ‘Simba Day’ kilipoanzishwa kwa ajili hiyo mashabiki hukutana kila Agosti 8 kila mwaka kwa ajili ya tukio hilo.
Kunogesha siku hiyo huchezwa mechi na wageni kutoka mipaka ya Tanzania ili kuleta burudani tosha, pia kuwa sehemu ya maandalizi ya kikosi kwa ajili ya msimu mpya.
Simba Day ya kwanza iliadhimishwa Agosti 8, 2009 jijini Dar es Salaam.Haruna Niyonzima akiwa na Jackson Mayanja. Ni miongoni mwa wachezaji watakaotambulishwa Agosti 8, 2017 kuwa miongoni mwa wachezaji wa Simba.
Haruna Niyonzima akiwa na Jackson Mayanja. Ni miongoni mwa wachezaji watakaotambulishwa Agosti 8, 2017 kuwa miongoni mwa wachezaji wa Simba.
Simba Day 2009 (Uhuru Stadium)
Simba ilicheza na SC Villa ya Uganda. Ilikuwa mechi ya kwanza kusheherekea siku yao ya kumbukumbu waliwatendea haki mashabiki na wapenzi wa klabu hiyo kwa ushindi mwembamba wa bao 1-0 lililofungwa na Hillary Echesa. Kocha alikuwa raia wa Zambia Patrick Phiri. Msimu huo Simba ilimaliza bila kupoteza mchezo wowote.
Simba Day 2010 (Uhuru Stadium)
Langoni alisimama Ally Mustafa ‘Barthez’ akilindwa na Haruna Shamte, Juma Nyosso, Amri Kiemba, Juma Nyosso, Amri Maftah dhidi ya Express ya Uganda. Mchezo huo uliochezwa dimba la Uhuru ulimalizika kwa sare tasa.
Simba Day 2011 (Sheikh Amri Abeid, Arusha)
Simba iliambulia kichapo cha bao 1-0 kutoka kwa Victors ya nchini Uganda. Mchezo huo ulichezwa katika dimba la Sheikh Amri Abeid jijini Arusha. Patrick Sembuya aliukwamisha mpira wavuni na kuwaacha Simba wakiwa vichwa chini.
Simba Day 2012 (Uwanja wa Taifa)
Ikiongozwa na Juma Kaseja, Felix Sunzu, Haruna Moshi ‘Boban’, Uhuru Selemani na wengineo walikubali kichapo cha mabao 3-1 kutoka kwa Nairobu City ya Kenya. Bao pekee la Simba SC lilifungwa na Sunzu huku ya wageni yakitupiwa na Duncan Owiti, Bruno Okullu, Boniface Onyango. Wakati huo Simba ilikuwa ikinolewa na kocha wa Serbia Milovan Cirkovic.
Simba Day 2013 (Uwanja wa Taifa)
SC Villa walipata nafasi kwa mara nyingine tena kurudi katika ardhi ya Tanzania katika Simba Day ambapo waliamulia kichapo cha mabao 4-1. Waliopeleka kilio hicho kwa Villa walikuwa ni Jonas Mkude, William Gallas na Betram Mwombeki alitupia mawili. Kikosi cha Simba kilikuwa kinanolewa Mtanzania Abdallah Kibadeni.
Simba Day 2014 (Uwanja wa Taifa)
Zesco ya Zambia iliwazabua Simba SC mabao 3-0 katika Simba Day. Waliopeleka kilio Msimbazi ni Jackson Mwanza katika dakika ya 14, Clatos Chane katika dakika 64 na katika dakika ya 90 Mayban Mwaka alipigilia msumari wa mwisho. Simba ilikuwa mikononi mwa kocha Zdravko Logarusic.
Simba Day 2015 (Uwanja wa Taifa)
Bao pekee la Simba lilifungwa na Awadhi Juma katika dakika ya 89 dhidi ya SC Villa ambao walipata nafasi ya kurudi tena kupambana na Simba. Kinachokumbukwa katika siku hiyo ni pale mashabiki waliokuwa wakianza kuondoka kwani walijua fika kuwa wameambulia patupu.
Simba Day 2016 (Uwanja wa Taifa)
Ilikuwa ikiadhimisha miaka 80 tangu kuanzishwa kwake. AFC Leopards ya Kenya ilikubali mwaliko dhidi ya Simba SC, ambapo walijipatia ushindi mnono wa mabao 4-0. Ibrahim Ajibu alitupia mawili, Jamal Mnyate na Shiza Kichuya. Siku hiyo mshambuliaji wa Ivory Coast Fredrick Blagnon na mlinzi wa kati Method Mwanjali wa Zimbabwe walitambulishwa.
Simba Day 2017 (Uwanja wa Taifa)
Mwaka huu wanacheza na Rayon Sport ya Rwanda wachezaji zaidi ya 10 watatambulishwa akiwamo Haruna Niyonzima, Emmanuel Okwi, John Bocco, Aishi Manula.

clouds stream