Wednesday, 14 December 2016

Nyayo za wanadamu wa kale zagunduliwa kaskazini mwa Tanzania

Nyayo hizo inakadiriwa ziliachwa na mwanamume aliyekuwa akitembea na kundi la wanawake na watoto

DAWID A. IURINO
Nyayo hizo inakadiriwa ziliachwa na mwanamume aliyekuwa akitembea na kundi la wanawake na watoto
img-20161130-wa0008

Nyayo zilizoachwa na binadamu wa kale mamilioni ya miaka iliyopita zimegunduliwa nchini Tanzania karibu na pahala ambapo nyayo sawa na hizo ziligunduliwa miaka ya 1970.

Alama hizo za miguu ziliachwa na binadamu wa kale walipotembea kwenye matope na majivu ya volkano yaliyokuwa hayajakauka.

Wataalamu wanakadiria kwamba viumbe ambao hujulikana kama Australopithecus afarensis, ndio walioacha nyayo hizo, na walikuwa na kimo na unene uliotofautiana.

Wanasayansi wanasema nyayo hizo zinaashiria jinsi binadamu wa kale walivyoishi.

Australopithecus afarensis ni miongoni mwa aina ya binadamu wa kale wanaofahamika zaidi na ambao waliishi kipindi kirefu.

Visukuku vya "Lucy", mwanamke kijana aliyeishi Ethiopia zaidi ya miaka 3.2 milioni, ndiye maarufu zaidi kutoka kwa kundi hilo la binadamu.

Nyayo hizo zilizogunduliwa huenda ziliachwa na mwanamume aliyekuwa labda anatembea na wenzake wa kike wadogo kwa kimo.

"Ushahidi huu mpya, ukiuzingatia pamoja na ushahidi wa awali, unaashiria kwamba binadamu wa kale walikuwa wanatembea kama kundi kwenye mandhari ambapo kulikuwa na matope, majivu na mawe ya volkano baada ya kulipuka kwa volkano na mvua kunyesha. Lakini kuna zaidi," amesema mtafiti mkuu Prof Giorgio Manzi, mkurugenzi wa mradi huo wa akiolojia nchini Tanzania.

"Nyayo za mmoja wa binadamu kati ya zile tulizogundua ni kubwa kuliko za wengine katika kundi hilo, jambo linaloashiria kwamba huenda alikuwa mwanamume.

"Kusema kweli, kimo cha 165cm ambacho kinadokezwa na nyayo hizo kinamfanya kuwa moja wa binadamu wa Australopithecus warefu zaidi kugunduliwa hadi wa leo."

Maisha kama ya sokwe

Mwaka 1976, nyayo zilizohifadhiwa ambazo zinaaminika kuachwa naAustralopithecus ziligunduliwa karibu na Laetoli, kaskazini mwa Tanzania, takriban kilomita 40 kutoka Olduvai Gorge.

Nyayo
Nyayo hizo ziliachwa kwenye majivu ya volkano

Nyayo hizo ambazo zinakadiriwa kuachwa miaka 3.66 milioni iliyopita, ni miongoni mwa nyayo za kale zaidi kugunduliwa duniani.

Sasa, ugunduzi wa kundi la sasa la nyayo umefichuliwa kwenye jarida la eLife.

Nyayo hizo ziligunduliwa wakati wa ufukuzi kwa ajili ya kujengwa kwa makumbusho eneo lililo mita 150 kusini mwa eneo ambalo ugunduzi wa kwanza ulifanywa.

Watafiti walioongoza uchunguzi huo, ambao wanatoka Italia na Tanzania, wanafikiri huenda nyayo hizo zina uhusiano, na zinaashiria mtindo wa maisha waAustralopithecus.

"Nadharia ambayo ni ya kuaminika ni kwamba kundi hilo labda lilikuwa na mwanamume mmoja, mwanamke mmoja au wawili au watoto, jambo ambalo linatufanya tuamini kwamba mwanamume huyo - alikuwa (alijamiiana) na wanawake zaidi ya mmoja," anasema Dkt Marco Cherin, mkurugenzi wa kitivo cha utaalamu wa mifupa ya kale katika Chuo Kikuu cha Perugia, Italia.

Ugunduzi huu unadokeza kwamba huenda mtindo wao wa kuishi ulikuwa "unakaribiana zaidi na wa sokwe kuliko sokwe-mtu au binadamu wa sasa," wanasema.

Nyayo hizo zinafanana na za mwanadamu
Nyayo nyingine zilizogunduliwa eneo hilo ni za twiga, faru na farasi wa kale

Miongoni mwa sokwe, sokwe dume na sokwe jike kadha huunda kundi la kujamiiana na kulea watoto.

Utafiti huo umeibua maswali kuhusu ni vipi na ni lini binadamu walipoanza kutembea wanavyotembea sasa.

Kutembea wima kwa miguu miwili

Australopithecus waliweza kutembea wakiwa wamesimama wima kwa miguu yao miwili, lakini hatujui walifanana kwa kiasi gani na binadamu wa sasa kwa jinsi walivyotembea.

Prof Robin Crompton wa Chuo Kikuu cha Liverpool, ambaye hakuhusika katika utafiti huo, anasema nyayo hizo zilizogunduliwa majuzi zitatoa maelezo zaidi, utathmini wa takwimu utakapofanyika.

"Baadhi ya watu wanasema walikuwa na mwendo tofauti kiasi, lakini sifikiri kwamba kuna ushahidi mzuri kuhusu hilo," ameambia BBC.

"Iwapo wanadamu wamekuwa wakitembea kwa mwendo sawa na wa sasa kwa zaidi au chini ya miaka 3.65 milioni, na mababu wa binadamu - katika kundi jingine la viumbe - Australopithecus - basi hilo linashangaza sana"

Eneo la Laetoli hupatikana kilomita 40 kutoka Olduvai Gorge
Eneo la Laetoli hupatikana kilomita 40 kutoka Olduvai Gorge

clouds stream