Saturday, 13 September 2014

Mashambulizi dhidi ya 'Dola la Kiislamu' yaiva


Mashambulizi dhidi ya 'Dola la Kiislamu' yaiva

Juhudi za Marekani kukusanya uungwaji mkono wa kimataifa kwa kampeni yake ya kijeshi dhidi ya kundi linalojiita "Dola la Kiislamu" zinaonekana kuendelea kuzaa matunda kwa washirika kadhaa kujiunga nazo.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, John Kerry (kushoto) katika mkutano na washirika wa mataifa ya Kiarabu.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, John Kerry (kushoto) katika mkutano na washirika wa mataifa ya Kiarabu.
Katika kile kinachoonekana kuwa matayarisho rasmi ya kulishambulia kundi hilo ndani ya ardhi ya Syria na Iraq, kufuatia hotuba ya jana ya Rais Barack Obama hapo jana, Rais wa Ufaransa amewasili Iraq hivi leo (12 Septemba), huku Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, John Kerry, akiendelea na ziara ya kusaka uungwaji mkono katika nchi za Kiarabu, nayo Australia ikitangaza hali ya tahadhari kutokana na uwezekano wa mashambulizi kutoka wanachama wa Dola la Kiislamu kwenye ardhi yake.
Ndege ya Rais Francois Hollande wa Ufaransa ikiwa na shehena ya tani 15 za msaada wa kibinaadamu utakaopelekwa mji mkuu wa Kurdistan baadaye leo, imewasili Baghdad, ikiwa ni ziara ya kwanza ya mkuu wa nchi tangu kutangazwa kwa serikali mpya nchini Iraq. Hollande anaambatana na waziri wake wa ulinzi, Jean-Yves Le Drian, na wa mambo ya nje, Laurent Fabius.
Juzi Jumatano, Fabius alitangaza nchi yake iko tayari kushiriki kwenye operesheni ya kijeshi ya Marekani dhidi ya kundi la Dola la Kiislamu, siku moja kabla hata Rais Obama hajatoa hotuba yake iliyofungua njia kwa mashambulizi hayo.
Wapiganaji wa Dola la Kiislamu waongezeka
Wapiganaji wa kundi la Dola ya Kiislamu ambao wanaripotiwa wakizidi kuongezeka.
Wapiganaji wa kundi la "Dola ya Kiislamu" ambao wanaripotiwa wakizidi kuongezeka.
Shirika la Ujasusi la Marekani (CIA) limesema huenda idadi ya wapiganaji wa kundi hilo ni mara tatu ya vile ilivyofikiriwa. Kufikia Agosti 2014, CIA inasema kundi hilo lilishakusanya takribani wapiganaji 35,000. Msemaji wa CIA, Ryan Trapani, amesema kiwango kikubwa cha wapiganaji walijiunga mwezi Juni baada ya mafanikio ya kundi hilo kwenye uwanja wa kivita na kutangaza utawala kwenye maeneo linaloyashikilia.
Hata hivyo, Ufaransa ambayo ilipinga uvamizi wa Marekani dhidi ya Iraq muongo mmoja uliopita, inasisitiza kuwa ushiriki wake utakuwa tu kwa maombi ya serikali ya Iraq. Kimsingi, hadi sasa Rais Hollande anahofia kuwa mkakati wa kuwashambulia waasi wa Dola la Kiislamu nchini Syria unaweza kumpa nguvu zaidi Rais Bashar al-Assad.
Kerry apata mafanikio
Irak Kurdische Peschmerga-Soldaten im Kampf gegen IS
Mpiganaji wa jeshi la Pashmerga la Kurdistan linalopambana na Dola la Kiislamu
Katika hatua nyengine, Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, John Kerry, amepata mafanikio kwenye kampeni yake ya kusaka uungwaji mkono wa mataifa ya Kiarabu kwenye uvamizi huu mpya.
Saudi Arabia, Bahrain, Kuwait, Oman, Qatar, Ufalme wa Nchi za Kiarabu, Misri, Iraq yenyewe, Jordan na Lebanon, zimekubali kuwa sehemu ya kile kinachofahamika kama "Muungano wa Wenye Nia" ya kulishinda kundi la Dola la Kiislamu, baada ya mazungumzo na Kerry mjini Jeddah, Saudi Arabia hapo jana.
"Mataifa ya Kiarabu yana nafasi muhimu sana kwenye muungano huo: uungaji mkono kijeshi, msaada wa kibinaadamu, kazi yetu ya kuzuia ufadhili wa kundi hili, na wapiganaji wa kigeni wanaohitajika na Dola la Kiislamu ili liweze kuwapo," alisema Kerry.
Australia yatangaza tahadhari ya ugaidi
Waziri Mkuu wa Australia, Tony Abbott.
Waziri Mkuu wa Australia, Tony Abbott.
Australia, ambayo ni sehemu ya nchi zinazoiunga mkono kampeni ya Marekani dhidi ya Dola la Kiislamu, imetangaza tahadhari ya kutokea kwa mashambulizi ya kigaidi, kutoka kwa raia wake waliorejea kutokea Syria na Iraq walikokuwa wakipigana upande wa waasi. Waziri Mkuu Tony Abbott amesema licha ya kutokuwepo undani wa taarifa za mashambulizi hayo, serikali yake imeamua kujiweka tayari.
"Vyombo vyetu vya usalama vimepandisha hali ya hadhari ya kitisho hicho kutokana na viashiria vilivyopo: idadi ya raia wa Australia ndani ya Mashariki ya Kari wanaopigana upande wa makundi ya kigaidi, idadi ya wale waliopo hapa wanaofahamika kuyaunga mkono makundi hayo," alisema Abbott.
Kwa upande wake Ujerumani imesema haitashiriki kwenye mashambulizi ya anga yatakayoongozwa na Marekani nchini Syria. Ujerumani inatoa msaada wa vifaa vya kijeshi kwa wapiganaji wa Kikurdi wanaopambana na wanamgambo wa "Dola la Kiislamu" kaskazini mwa Iraq.
Tayari Syria imeshashema kuwa itachukulia mashambulizi yoyote yatakayofanyika kwenye ardhi yake bila ya mashauriano kuwa ni kitendo cha uchokozi wa makusudi.
Mwandishi: Mohammed Khelef/ape/afpe
Mhariri: Daniel Gakuba

clouds stream