Sunday, 12 November 2017
Taarifa Muhimu Kutoka Bodi Ya Mikopo Kwa Wanafunzi Elimu Ya Juu
Mkurugenzi Mtendaji wa HESLB, Abdul Razaq Badru
Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB) imetangaza orodha nyingine yenye wanafunzi 1,775 wa Mwaka waKwanza waliofanikiwa kupata mikopo na hivyo kufanya jumla ya wanafunzi wa mwaka wa kwanza waliopangiwa mikopo hadi sasakufikia 31,353.
Katika Awamu ya Kwanza, wanafunzi 10,196 wa mwaka wa kwanza walipangiwa mikopo, Awamu ya Pili wanafunzi 11,481, nasasa Awamu ya Tatu wanafunzi 7,901.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa jana (Jumapili, Novemba 12, 2017) na Mkurugenzi Mtendaji wa HESLB Bw. Abdul-Razaq Badru, orodha kamili ya wanafunzi hao inapatikana katika tovuti ya Bodi (www.heslb.go.tz) na pia imetumwa kwa vyuo husika jana ili kuwawezesha wanafunzi kufanya usajili na kuendelea na masomo.
“Tumekua tukifanyia kazi orodha za udahili ambazo tumekuwa tukipokea, na kila tunapokamilisha, tunatoa orodha za wanafunzi waliopangiwa mikopo ambao wana sifa – leo tumetoa hao 1,775,” amesema Badru.
Aidha, Badru amekumbusha kuwa kiasi cha shilingi bilioni 427.54 zimetengwa kwa ajili ya mikopo ya wanafunzi kwa mwaka 2017/2018 na tayari Serikali imeshatoa shilingi 147.06 bilioni kwa ajili ya robo ya kwanza ya mwaka huu wa 2017/2018.
Fedha hizo, shilingi bilioni 427.54, ni kwa ajili ya jumla ya wanafunzi 122,623 wa mwaka wa kwanza na wale wanaoendelea na masomo.
Wakati huohuo, HESLB imetangaza kufungua dirisha la rufaa kuanzia leo, Jumatatu, Novemba 13, 2017 hadi Novemba 19, 2017 ili kuwapa fursa waombaji wote ambao hawajaridhika na upangaji wa mikopo kuwasilisha rufaa kupitia vyuo walivyopata udahili.
Kwa mujibu wa Mkurugenzi Mtendaji huyo wa HESLB, lengo la HESLB ni kuhakikisha wanatangaza orodha ya majina ya waombaji mikopo waliofanikiwa katika rufaa zao ifikapo au kabla ya tarehe 30 Novemba mwaka huu.
“Tunatoa wito kwa uongozi wa vyuo vyote kupokea maombi ya rufaa za wanafuzi na kuwasilisha kwa Bodi ya Mikopo kabla ya Novemba 22, 2017 ili kuiwezesha Bodi kutoa orodha ya waombaji waliofanikiwa katika rufaa zao ifikapo Novemba 30, 2017,” amesema Badru katika taarifa yake.
Maelezo ya kina kuhusu utaratibu wa kuwasilisha rufaa yatatolewa kupitia tovuti ya Bodi (www.heslb.go.tz).
Mgomo Mabasi Mikoani Wanukia, Wananchi Waaswa Kutokata Tiketi
Taswira nzima ya mabasi yaendayo Mikoani na Nchi Jirani katika Kituo cha Ubungo.
Chama cha Wamiliki wa Mabasi yaendayo Mikoani na Nchi Jirani Tanzania (TABOA), kimewataka wananchi kutokata tiketi za kusafiri kwa siku ya kesho, Jumanne, kufuatia mgomo wa mabasi hayo.
Katibu Mkuu wa TABOA, Enea Mrutu amesema hayo kupitia Mkutano Mkuu Maalum wa TABOA na kudai kuwa maamuzi ya mgomo huo ni katika kuwashinikiza wabunge kutopitisha sheria kandamizi dhidi ya wamiliki wa mabasi.
Amesema sheria hiyo ni kandamizi kwakuwa inashindwa kutofautisha kosa la mmiliki wa basi na dereva.
“Tunaomba radhi wateja wetu wote kwa kuwanyima huduma lakini kimsingi sheria hiyo ndiyo inayowanyima huduma,” amesema.
Ameongeza kuwa vita yao kubwa ni sheria ambayo haikutenganisha makosa baina ya dereva na mmiliki wa chombo husika na kupelekea kumfunga mmliki kwa kosa linalomhusu dereva.
“Tulisema sheria hiyo ibainishe makosa ili kosa linalomhusu dereva liende kwa dereva na lile linalomhusu mmiliki liende kwa mmiliki lakini wenzetu hawakusikia hivyo tumesema watu wasikate tiketi na Jumanne ndio mwisho wa kutoa huduma,” amesisitiza.
Lema Atoa Ushauri Kuhusu ‘Wabunge Wa Lipumba’
Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema.
Mbunge wa Arusha Mjini, Mhe. Godbless Lema amemshauri Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Job Ndugai kutumia busara kuwaondoa bungeni wabunge nane walioingia bungeni kuziba nafasi za wabunge nane waliokuwa wamevuliwa uanachama wa Chama cha Wananchi (CUF) Julai 24, mwaka huu.
Lema ametoa ushauri huo kupitia mtandao wake wa kijamii ikiwa ni siku chache tu baada ya Mahakama Kuu kutengua uamuzi wa
kufukuzwa kwa Wabunge 8 na Madiwani 2 wa CUF mpaka pale shauri la msingi litakaposikilizwa.
“Mh Spika anapaswa kuzingatia kwa busara uamuzi uliotolewa na mahakama kwa kuwaondoa wale Wabunge wa Lipumba ndani ya Bunge na kuwarejesha Wabunge halali sasa, mpaka hapo haki itakaposhinda zaidi,”ameandika Lema.
Wabunge hao nane walivuliwa uanachama Julai 24 na Baraza Kuu la Uongozi la Taifa la Chama cha Wananchi, CUF linaloongozwa na Prof. Lipumba kwa madai ya utovu wa nidhamu yakiwemo kukisaliti chama hicho na Tume ya Uchaguzi (NEC) kuteua wabunge wengine kutokana na uamuzi huo na kuchukua nafasi zao maramoja.
Subscribe to:
Posts (Atom)