Thursday, 2 November 2017
NASA Kuanza Maandamano Kupinga Serikali Ya Kenyatta
Muungano wa Upinzani nchini Kenya (NASA) umesema kuwa una mpango wa kuanza kufanya maandamano kuanzia wiki ijayo yenye lengo la kuonyesha kutoitambua serikali.
Hili linajiri siku chache baada ya Taifa hilo kufanya uchaguzi wa marudio uliofanyika Oktoba 26, mwaka huu na kususiwa na Mgombea wa NASA, Raila Odinga na kushuhudiwa Rais, Uhuru Kenyatta akitangazwa kuwa mshindi na Rais Mteule wa Kenya.
Aidha,NASA imepanga orodha ya bidhaa na huduma zitakazo susiwa na wafuasi wake ikiwa ni pamoja na majengo ya kibiashara ambayo yametundikwa picha ya Rais Kenyatta na kuamuru wafuasi wake wasifanye biashara ama miamala na benki moja maarufu nchini humo.
Hatahivyo, Viongozi wa Jubilee wamemtaka kinara wa NASA, Raila Odinga kulegeza msimamo wake ili kulisaidia taifa hilo kusonga mbele.
NASA wamesema maandamano hayo yatakuwa ya amani na wametoa mafunzo kwa watu watakaoyaongoza ili yasidhuru
wananchi wengine.