Sahara Media Group Yaijibu TCRA, Kufungiwa Star Tv
Tarehe January 17, 2016
Kampuni ya Sahara Media Group inayomiliki Star Tv, RFA na Kiss Fm imebuka na kuishangaa mamlaka ya mawasilano Tanzania TCRA iliyoitaka kampuni hiyo kufunga vyombo vyake vyote vya habari.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa jana na TCRA imevitaja vyombo vya habari 21 ikiwemo Star TV, Redio Free Afrika na Kiss FM kwa madai ya kutolipia ada ya leseni.
Wakizungumzia kufungiwa na TCRA Manejimenti ya sahara media group imesema kuwa haijapata barua au taarifa rasmi yeyote kutoka TCRA ya kutakiwa kufunga vyombo vyake.
Imesema wameshtushwa na taarifa hiyo ikizingatiwa kwamba wamekuwa wakilipia leseni ada zake na ada za masafa kwa kiasi cha zaidi ya shilingi milioni 500 hadi kufikia mwezi October 2015.
Wamesema yamekuwapo mawasiliano ya mara kwa mara kati ya TCRA kanda ya Mwanza, makao makuu na sahara media group limited nakukubaliana juu ya utaratibu wa malipo ya ada husika.
Hata hivyo menejimenti imeshangazwa na hatua hiyo ya TCRA kutangaza kuvifungia vituo vyake kupitia mkutano wa vyombo vya habari bila kujali athari za kufungia vyombo vya kitaifa kwa walaji na watoa huduma.
Sahara media group limited imekuwa ikilalamikia utozwaji wa ada kwa dola za kimarekani jambo ambalo limekuwa likipandisha ada hizo kila mara na kufanya ulipwaji wa ada hizo kibajeti kukwama kwama.
Menejimenti pia imelaani taarifa hiyo kutolewa mwishoni wa wiki na kuvipa vituo husika siku mbili tu kukamilisha ulipaji ada wakijua dhahiri jumamosi na jumapili sio siku za kazi.
Menejimenti ya star tv imewaondoa wasiwasi watazamaji na wasikilizaji wake kufuatia kuanza kulishughulikia suala hilo kati yake na TCRA.