CUF Wagoma, CCM ‘Mbele Kwa Mbele’ Uchaguzi Mkuu Zanzibar
Tarehe January 28, 2016
Chama cha Wananchi (CUF) kimetangaza rasmi kutoshiriki marudio ya uchaguzi wa Zanzibar unaotarajiwa kufanyika Machi 20 mwaka huu huku Chama cha Mapinduzi (CCM) kikiwataka wanachama wake kujiandaa kwa uchaguzi wa marudio.
Katibu Mkuu wa Chama hicho, Maalim Seif Hamad amewaambia waandishi wa habari leo kuwa baada ya Baraza Kuu la Uongozi la Taifa la CUF kujadili tamko la Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar, Jecha Salum Jecha, la kuitisha uchaguzi wa marudio tarehe 20 Machi, wametoa azimio la kukataa moja kwa moja kushiriki uchaguzi huo waliouita ‘batili’.
“Chama Cha Wananchi (CUF) hakitoshiriki katika uchaguzi wa marudio uliopangwa kufanyika tarehe 20 Machi, 2016 kwa sababu uchaguzi huo si halali kwani uchaguzi halali ulishafanyika,” imesomeka sehemu ya maazimio hayo.
Baraza hilo limesema uchaguzi mkuu wa Zanzibar ulikwishafanyika tarehe 25 Oktoba 2015 na washindi wa Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi na Madiwani kupewa shahada za kuwathibitisha na kuwatambua kama washindi halali.
CUF wameziomba jumuiya za kimataifa na taasisi zinazosimamia haki za binadamu na zinazopambana na makosa ya jinai kimataifa ikiwemo Mwendesha Mashtaka wa Mahakama ya Kimataifa ya Makosa ya Jinai (International Criminal Court – ICC) kufanya uchunguzi wa hali ilivyokuwa wakati wa uchaguzi ili kupata majibu ya kinachoendelea visiwani Zanzibar.
Vilevile baraza hilo limetoa wito kwa wazanzibari kutoshiriki uchaguzi huo usio halali wa marudio.