Nape Alia Na Lowassa, Ataka Chadema Imngo’e
Tarehe January 14, 2016
Katibu wa Itikadi na Uenezi Nape Nnauye amekitaka chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kimfukuze aliyekuwa mgombea urais Edward Lowassa ili kuonesha kuwa kweli wana dhamira ya dhati ya kupambana na ufisadi.
Akizungumza na Waandishi wa Habari jijini hapa Nape alisema Chadema waliachana na ajenda ya ufisadi mara baada ya kumpokea mwanasiasa Edward Lowassa aliyekuwa anatuhumiwa kwa ufisadi katika sakata la Richmond.
Amesema CCM haikumpitisha Lowassa kugombea urais kwa sababu ya ufisadi sababu iliyopelekea aamue kuhama CCM na kutimkia Chadema.
Nape amesema hayo akimjibu Mwanasheria mkuu wa Chadema Tundu Lissu ambaye juzi alisema kuwa ufisadi ni ajenda ya kudumu ya Chadema kwa madai kuwa Rais Magufuli hawezi kuufumua wote katika uongozi wake.
Katibu huyo wa Itikadi amesema ajenda ya ufisadi ndiyo ilikibeba chama hicho katika uchaguzi mkuu ndio sababu ya Dkt. John Magufuli kuibuka mshindi akimuacha kwa mbali mpinzani wake Edward Lowassa.