Waziri wa Mambo ya Ndani ya nchi Mwigulu Nchemba.
Waziri wa mambo ya Ndani ya nchi Mwigulu Nchemba amemtaka IGP Ernest Mangu kumchukulia hatua Askari aliyemtisha Nape Nnauye kwa Bastola jana wakati anazungumza na Waandishi wa habari jijini hapa.
Kupitia taarifa yake kwenye ukurasa wake wa mtandao wa kijamii Nchemba amesema tukio lile halikuwa sahihi na kuagiza hatua zichukuliwe kwa kuwa Nape Nnauye si jambazi, hakuwahi kuwa na taarifa za uhalifu, sasa kwanini mtu amtishe kwa bastola tena mbele ya umati mkubwa uliojaa waandishi wa habari.
“Mh.Nape Moses Nnauye sio jambazi, ni mtanzania, ni Mbunge, mjumbe wa NEC wa CCM, hana record ya uhalifu. Kitendo cha mtu kumtolea Bastola, Sio cha ki asikari, sio cha kitanzania na sio cha ki Mungu, kama mtu ameweza kutoa Bastola mbele ya Kamera nawaza mbali ingekuwa kwenye uchochoro angefanya nini.”
Aidha, Waziri Nchemba amesema kuwa amemuagiza Mkuu wa Jeshi la Polisi Nchini (IGP), Ernest Mangu kumbaini mtu huyo aliyefanya kitendo hicho na kumchukulia hatua stahiki.