Thursday, 13 April 2017
Trump abadili msimamo kuhusu NATO na kusema shirika hilo sasa linafaa
Rais wa Marekani Donald Trump amesema kuwa shirika la kujihami la NATO sasa linafaa na kwamba halijapitwa na wakati hatua ambayo imewashangaza washirika wake.
Akizungumza na katibu mkuu wa shirika hilo Jens Stoltenberg katika Ikulu ya Whitehouse ,Trump amesema kuwa tishio la ugaidi limesistiza umuhimu wa muungano huo.
Ametoa wito kwa NATO kusaidia washirika wake nchini Iraq na Afghanistan.
Bwana Trump mara kwa mara amekuwa akitilia shaka umuhimu wa shirika hilo huku akilalamika kwamba Marekani inatoa kitita kikubwa cha ufadhili wake ikilinganishwa na mataifa mengine.
Sio mara ya kwanza kwa bwana Trump kulalamika kuhusu shirika hilo siku ya Jumatano.
Katika mahojiano na jarida la Wall Street alisema kuwa hataitaja China kuwa imekuwa ikishawishi sarafu yake ili kuangazia maslahi yake ,licha ya kuahidi kusema hivyo siku moja tu baada ya kuchukuwa mamlaka.
Katika mahojiano ya pamoja ya vyombo vya habari na Stoltenberg Bwana Trump alisema: katibu mkuu wa Nato na mimi tumefanya mazungumzo ya kufana kuhusu ni nini zaidi NATO inaweza kufanya katika vita dhidi ya ugaidi.
Nililalamika kuhusu hilo hapo awali na wakafanya mabadiliko na sasa wanakabiliana na ugaidi.
Nilisema NATO 'imepitwa na wakati' lakini sasa 'haijapitwa na wakati'.
Bwana Trump alisisitiza wito wake kwa wanachama wa NATO kuchanga fedha zaidi kwa shirika hilo.
Wednesday, 12 April 2017
UEFA: Barcelona yabamizwa na Juventus 3-0 Klabu Bingwa
Juventus waliwapa kisago Barca
Barcelona imechabangwa magoli matatu kwa sufuri na Juventus katika mchezo wa kwanza wa robo fainali ya Klabu Bingwa Ulaya.
Paulo Dybala alifunga magoli mawili katika dakika ya 7 na ya 22. Bao la tatu lilifungwa na Giorgio Chiellini katika dakika ya 55.
Barcelona walicheza kufa na kupona kujaribu kupata japo bao moja la ugenini lakini hawakuweza kufua dafu.
Mchezo mwingine wa robo fainali kati ya Borussia Dortmund dhidi ya Monaco uliahirishwa baada ya basi ya Dortmund kushambuliwa.
Mchezo wa marudiano ni wiki ijayo.
Basi la timu ya B. Dortmund lakabiliwa na milipuko Ujerumani
Gari la Dortmund lililengwa na milipuko mitatu
Polisi nchini Ujerumani imesema kuwa gari lililokuwa limewabeba wachezaji wa Borussia Dortmund kuelekea katika mchezo wa nyumbani kwenye ligi ya mabingwa Ulaya lililengwa na milipuko mitatu.
Katika mkutano na waandishi wa habari, wamesema kuwa barua ilikutwa pembezoni mwa eneo la shambulizi hilo,lakini haikuwa na maelezo ya kutosha.
Polisi imekana kuwa ni shambulizi la kigaidi.
Mchezaji mmoja wa Dortmund na raia wa Uhispania Marc Bartra amejeruhiwa na kufanyiwa upasuaji.
Mlinzi Marc Bartra amejeruhiwa katika shambulizi hilo
Taarifa za kiintelijensia zinasema kuwa zinachunguza shambulizi hilo kama linahusika na mashabiki wa timu ya upinzani.
Mchezo kati ya Dortmund na Monaco umeahirishwa mpaka Jumatano.
JPM Kuweka Jiwe La Msingi Ujenzi Reli Ya Kisasa ‘Standard Gauge’ Leo
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John pombe Magufuli leo anatarajia kuweka jiwe la msingi kwa ajili ya ujenzi wa Reli ya kisasa (Standard Gauge) katika eneo la Pugu Jijini Dar es salaam.
Hayo yamesemwa na Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam, Paul Makonda alipotembelea eneo la mradi huo lililopo Pugu Jijini Dar es salaam na kudai kuwa mradi huo utazalisha ajira nyingi katika kada mbalimbali.
Aidha, ameongeza kuwa mradi huo utakapo kamilika utarahisisha usafiri wa kutoka Dar es salaam hadi katika mikoa ya Morogoro, Dodoma na Mwanza.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa Kampuni ya Reli (RAHCO), Masanja Kadogosa amesema kuwa kukamilika kwa ujenzi huo kutarahisisha shughuli za usafiri na usafirishaji kwa kuwa safari ya Dar es salaam hadi Morogoro itatumia muda wa saa 1:16, huku Dar es salaam hadi Dodoma itatumia masaa 2:30 na safari ya Dar es salaam hadi Mwanza itatumia masaa 7:30.
Mradi huo ambao uko chini ya Kampuni za Merkezi ya Uturuki na MotaEngil Afrika ya Ureno, kwa awamu ya kwanza utaanza na kipande cha kilomita 300 kati ya Dar es salaam hadi Morogoro kwa gharama zaidi dola bilioni moja za Marekani.
Trump Aionya Tena Korea Kaskazini, Adai Inatafuta Matatizo
Meli ya Carl Vinson kwa sasa inaelekea rasi ya Korea.
Rais wa Marekani Donald Trump kwa mara nyingine tena ametoa onyo dhidi ya Korea Kaskazini kupitia mtandao wa twitter, akisema kuwa Pyongyang inatafuta matatizo.
Pia ameitaka China ambayo ni mshirika mkuu wa Korea Kaskazini kujaribu kukabiliana na jirani wake huyo.
Bwana Trump alipendekeza kuwa China itapata makubaliano bora ya kibiashara ikiwa itafanya hivyo, lakini akaongeza kuwa Marekani haitaogopa kutatua tatizo la Korea Kaskazini bila ya Uchina.
Trump alitoa matamshi kama hayo wiki moja iliyopita lakini tangu wakati huo msukosuko umekuwa mkubwa.
Marekani imetuma meli za kivita kuelekea rasi ya Korea hatua ambayo imeikasirisha Korea Kaskazini.
Thabo Mbeki Aunga Mkono Wanaompinga Zuma.
Thabo Mbeki
Aliyekuwa Rais wa Afrika Kusini, Thabo Mbeki amewataka wabunge wa chama tawala cha ANC kutenda yanayowafaa raia wa nchi hiyo na sio kile kitakachofaidisha chama wakati wa kujadili mswada wa kutokuwa na imani na Rais Jacob Zuma, wiki ijayo.
Wito wa Mbeki huenda ukawakera wanaomuunga mkono Zuma ambao wameapa kuupinga mswada huo vikali bungeni, kulingana na tovuti ya IOL.
Upinzani unadai kuwa Zuma ni fisadi na kwamba alimfuta kazi aliyekuwa Waziri wa Fedha, Pravin Gordhan licha ya kuwa Gordhan aliheshimika sana.
Wadadisi wa mambo wanasema hatua hiyo ya Zuma ilikuwa kwa ajili ya kuchukua usukani katika wizara ya fedha.
Hatahivyo, Zuma anakanusha madai hayo ya ufisadi na kudai kuwa yeye kufanya mabadiliko katika baraza la mawaziri na ni kwa manufaa ya raia.
Kulingana na tovuti hiyo, Mbeki amesema kuwa wabunge wanafaa kuwa sauti ya wananchi na wala sio sauti ya vyama vya kisiasa.
Anasema huu ni wakati wa Afrika Kusini kujua ukweli kuhusu uhusiano wa kikatiba kati ya wananchi na viongozi wao wa kisiasa.
Tuesday, 11 April 2017
Arsenal walala 3-0 mbele ya Crystal Palace
Kipindi cha pili Arsenal hawakupiga shuti lililolenga lango la Palace
Crystal Palace imeendelea kurudisha matumaini ya kusalia kwenye ligi kuu ya England baada ya kuichapa Arsenal ambayo nayo inahaha kuingia nafasi ya nne baada ya kukumbana na wakati mgumu.
Iwapo Arsenal itashindwa kuingia nafasi nne bora, itakuwa ni mara ya kwanza tokea imeanza kunolewa na Arsene Wenger mwaka 1996.
Palace wameshinda kwa magoli 3-0 katika mchezo uliokuwa wa kusisimua.
Rais Zuma: Waandamanaji ni wabaguzi wa rangi
Rais wa Afrika Kusini Jacob Zuma
Rais wa Afrika Kusini Jacob Zuma amewataja watu wanaofanya maandamano dhidi yake kuwa wabaguzi wa rangi akisema walibeba mabango yalioonyesha kuwadharau watu weusi.
Maelfu ya waandamanaji walifanya maandamano baada ya kumfuta kazi waziri wake wa fedha Pravin Gordan.
Maandamano hayo yalipangwa na vyama kadhaa vya upinzani na makundi kadhaa ya wanaharakati.
''Maandamno yaliofanyika wiki iliopita yalibaini kwamba ubaguzi wa rangi upo na unaendelea nchini Afrika Kusini'', alisema.
Wakati huohuo wafuasi wa rais wa Afrika Kusini Jacob Zuma walivuruga hafla ya makumbusho ya aliyekuwa mwanaharakati wa kupambana na ubaguzi wa rangi, Ahmed Kathrada.
Watu hao walianza kuleta uzushi wakati aliyekuwa waziri wa fedha Pravin Gordan alipokuwa anatoa hotuba yake ambayo ilikuwa inakashifu ufisadi katika chama cha ANC, akisema kuwa huenda chama hicho hakitashinda uchaguzi wa 2019.
Umati ulianza kuimba nyimbo za kumsifu Zuma ambaye amekumbwa na kashfa baada ya nyingine.
Hafla hiyo ya Kathrada ilikuwa ikiendelea KwaZulu-Natal ambapo umati huo ulimsifu rais Zuma kwa kumpiga kalamu Gordan.
Akijaribu kuipaza sauti yake juu ya kelele wa umati, Gordan alisema, " ikiwa tutaendelea kuzozana tutapoteza imani ya watu wa Afrika Kusini kwetu.
Tunataka kubaki serilkalini ili tuibadilishe Afrika Kusini."
Wiki ijayo, Zuma anatarajiwa kupambana na kura ya kutokuwa na imani dhidi yake ambayo inafadhiliwa na upinzani.
Anadaiwa kuwa kiongozi fisadi ambaye anataka kuwajaza rafiki zake kwenye wizara ya fedha.
Rafiki zake Zuma hata hivyo wanakanusha madai hayo huku wakisema kuwa Zuma ana nia tu ya kuendeleza mabadiliko makubwa ya kiuchumi itakayonufaisha nchi.
Mahakama ilitoa amri mwaka jana ikisema kuwa Zuma alivunja kiapo chake cha kazi kwa kukosa kulipa serikali pesa zilizotumiwa kuboresha makazi yake ya kibinafsi na kutaka ashtakiwe kwa kosa la ufisadi.
Zuma anasema yeye hana makosa yoyote.
ROMA AVUNJA UKIMYA SAKATA LA KUTEKWA MBELE YA MWAKYEMBE
Mwanamuziki Roma Mkatoliiki alipozungumza na Waandishi wa Habari kuhusiana na sakata la kutekwa nyara.
Mwanamuziki Roma Mkatoliki hatimaye leo ametoa ya moyoni kufuatia yeye na wasanii wenzake 2 pamoja na mfanyakazi wa ndani kutekwa na kuteswa na watu wasiojulikana siku ya Jumatano wiki iliyopita katika Studio za Tongwe jijini Dar es salaam na kupatikana Jumamosi wiki iliyopita.
Akizungumza na Waandishi wa Habari kwenye ukumbi wa Idara ya Habari maelezo leo Roma amesema walikuja watu waliokuwa na silaha za moto, wakawaamuru kuingia kwenye gari na kisha wakafungwa vitambaa usoni na pingu mkononi na kupelekwa eneo ambalo hawajalijua hadi sasa.
Amesema baada ya kufikishwa katika eneo hilo waliteswa ikiwemo kupigwa pamoja na kuhojiwa kwa muda wa siku tatu mfululizo, hivyo kupata maumivu makali kwenye miili yao.
Roma amesema kuwa mpaka sasa hawana uhakika na usalama wao kwa kuwa mahali walipokuwa hapakuwa pazuri.
“Kama alifanyiwa daktari, baadaye akafanyiwa msanii, usishtuke kesho akafanyiwa mwandishi wa habari, au Mbunge.”Alisema Roma.
Hata hivyo Roma ameacha maswali mengi ikiwemo nini sababu ya kutekwa kwao na watu gani waliohusika na utekaji huo pamoja na kuwapa mateso makali.
Katika mitandao ya kijamii inadaiwa kuwa wimbo uliopelekea wasanii hao kutekwa ni ule unaoitwa ‘Tanzagiza’ulioimbwa na msanii Sifa Digital video yake ipo Youtube.
Aidha katika mkutano huo Roma aliambatana na Waziri Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dkt. Harrison Mwakyembe kama waziri mwenye dhamana ya Wasanii na kazi zao ambapo kwenye mkutano huo alisema alipata hofu kusikia Roma ametekwa na watu wasiojulikana hivyo amehudhuria ili afahamu nini kilitokea.
Baadhi ya watu kwenye mitandao ya kijamii wamedai kuwa Roma ameshindwa kuelezea ukweli wa kile kilichotokea kutokana na kuhofia usalama wake kwa sasa ikiwa ni miezi minne tangu msaidizi wa Freeman Mbowe Ben Saanane atekwe na haijulikani alipo hadi sasa.
Wednesday, 5 April 2017
Korea Kaskazini yafyatua kombora kwenda bahari ya Japan
kombora lililorushwa na Korea Kaskazini
Japan imeijibu vikali Korea Kaskazini kufuatia nchi hiyo kufyatua kombora jingine hivi karibuni na kutaja hilo ni tatizo kubwa lililopindukia.
Katika Mji wa Pyongyang,Kombora lenye uzito wa kati lilirushwa upande wa mashariki mwa bandari ya Sinpo kuelekea bahari ya Japan.
Waziri kiongozi wa nchi hiyo ,Yoshihide Suga amewaambia waandishi wa habari kuwa nchi yake haiwezi stahimili vitendo hivyo vya uchochezi ambavyo Korea kaskazini imevirudia kuvifanya.
Kombora hilo limerushwa siku chache kabla ya rais wa China, Xi Jinping kufanya ziara nchini Marekani kukutana na rais Trump ili kujadili namna ya kudhibiti mipango ya Nuklia na makombora ya masafa marefu ya Korea kaskazini.
Chama cha wafanyikazi chamtaka Zuma kujiuzulu
Wafanyikazi wa COSATU Afrika Kusini wamtaka Zuma Kujiuzulu
Chama kikubwa cha wafanyikazi nchini Afrika Kusini, Cosatu kimeunga mkono kauli ya wale wanaomtaka rais Jacob Zuma kujiuzulu.
Japo Cosatu kinajulikana kuunga mkono chama tawala ANC, kimemshutumu rais Zuma kwa kile wanachokitaja kuwa na uhusiano wa karibu mno na familia moja ya jamii ya Wahindi huko Afrika Kusini, waitwao Gupta, wanaodaiwa kuwa na ushawishi mkubwa katika serikali ya Zuma.
Bw. Zuma na falimia hiyo ya Guptas, wamekana kufanya kosa lolote.
Wiki iliyopita chama chengine mshirika wa ANC The South African communist party pia kilimtaka Bw. Zuma kung'atuka mamlakani kutokana na kashfa tele zinazozidi kumuandama, madai ya makosa ya ufisadi.
Sarafu ya Rand imekuwa ukiyumba yumba kutokana na malumbano hayo ya kisiasa nchini Afrika Kusini hasa tangu kufutwa kazi kwa aliyekuwa waziri wa fedha nchini humo Pravin Gordhan.Pravin Gordhan akihutubia umma
Rais Jacob Zuma amedhoofishwa kisiasa zaidi ya ilivyokuwa awali.
Wito wa Cosatu wa kumtaka kujiuzulu ni pigo kubwa kwa kiongozi huyo wa taifa.
Chama chicho cha wafanyikazi kimekuwa kikimuunga mkono dhidi ya wito wa kumtaka kung'atuka mamlakani.
Macho yote sasa yanaelekezwa katika kamati ya kazi ya chama cha ANC ambacho kinafanya mkutano.
Hatahivyo licha ya uamuzi wowote utakaoafikiwa katika mkutano huo unaondelea, mgawanyiko mkali uliopo katika chama hicho utazidi kati ya wale wanaomuunga mkono Zuma na wapinzani wake.
Bwana Zuma anatarajiwa kuondoka mamlakani mwaka 2019 mwisho wa muhula wake wa pili kama rais wa taifa hilo.
Wiki iliopita,naibu wa rais Cyril Ramaphosa alipinga kufutwa kazi kwa bwana Gordhan
Whatsapp Kuja Na Huduma Ya Fedha Kwa Njia Ya Mtandao
Mtandao wa WhatsApp, ambao unatoa huduma ya kutuma ujumbe kwa haraka zaidi duniani hivi karibuni utawaruhusu makumi kwa mamilioni ya watumiaji wake kutuma kitu muhimu zaidi ya ujumbe, picha ama video yaani fedha.
WhatsApp inailenga zaidi huduma hiyo nchini India ambako kuna soko lake kubwa zaidi na kuangalia uwezekano wa kuingia katika malipo ya mtandaoni.
Programu hiyo inayomilikiwa na Facebook, inaajiri Mkurugenzi wa kuongoza jitihada hizo za malipo ya dijitali katika nchi hiyo ya Kusini mwa Asia.
Huduma hiyo itashirikiana na mabenki katika kusaidia miamala ya kidijitali kwa kutumia WhatsApp.
India ina watumiaji wa WhatsApp zaidi ya milioni 200 kila mwezi ambayo ni moja ya tano ya watumiaji wake wote hivyo si jambo la kushangaza kuona imelengwa yenyewe kwanza.
Subscribe to:
Posts (Atom)