Monday, 9 May 2016
TAKUKURU Yakamata Tani 4,900 Za Sukari Iliyofichwa Mbagala Na Tabata
TAKUKURU Yakamata Tani 4,900 Za Sukari Iliyofichwa Mbagala Na Tabata
Tarehe May 8, 2016

Taasisi ya kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) imebaini uwepo wa tani 4,579.2 za sukari iliyofichwa baada ya kununuliwa kutoka Kiwanda cha Sukari Kilombero.
Kwa mujibu wa Taarifa iliyotolewa leo Jijini Dar es salaam na Mkurugenzi Mkuu wa TAKUKURU, Valentine Mlolowa, taasisi hiyo imeanza uchunguzi dhidi ya swala hilo kwa kushirikiana na Jeshi la Polisi.
Mei 5, 2016 timu ya uchunguzi ilitembelea maghala yaliyopo Tabata Jijini Dar es salaam na kubaini uwepo wa sukari hiyo.
“TAKUKURU tayari imetembelea Maghala ya mfanyabiasha Haruni Daudi Zacharia ambaye ni Mkurugenzi Mtendaji wa Al-Naeem yaliyoko Mbagala na Tabata ambaye ni miongoni mwa wafanyabiashara wakubwa wa sukari hapa nchini na anayetuhumiwa kuficha bidhaa hiyo,” imesema sehemu ya taarifa hiyo.
Aidha uchunguzi uliofanywa na Taasisi hiyo umebaini kuwepo kwa njama za dhati za kutouza sukari iliyokutwa katika maghala hayo kulikofanywa na mfanyabiashara huyo kwani hata sehemu ya maghala ilipokutwa sukari hiyo hapakuwa na dalili za upakiaji wa sukari hiyo ili iweze kusambazwa.
Taarifa hiyo imeendelea kufafanua kuwa katika eneo la Kitumbini kumekuwa na wananchi wengi wanaohitaji bidhaa hiyo na wachache sana waliweza kuuziwa licha ya ukweli kwamba sukari ilikuwepo.
Katika uchunguzi wake, TAKUKURU pia imebaini kuwepo kwa mikakati ya dhati iliyokuwa ikifanywa na mfanyabiasha huyo kwa kununua sukari yote toka viwanda vya ndani na kisha kuihifadhi na kuuza bidhaa hiyo kidogo kidogo kwa wastani wa tani 250 kwa siku wakati alikuwa na uwezo wa kuuza zaidi jambo lililochangia uhaba wa sukari katika soko.
“Kuficha bidhaa ni kosa la uhujumu uchumi na ni kinyume na Aya ya 3 Jedwali la kwanza Sheria ya Uhujumu Uchumi Sura ya 200 [Chapisho la Mwaka 2002] na Serikali haitavumilia hujuma za namna hii na itachukua hatua kali dhidi ya mfanyabiashara yeyote ataekwenda kinyume na sheria hii,” imesisitiza taarifa hiyo.
TAKUKURU inatoa wito kwa wafanyabiashara wote wa sukari kuacha vitendo vya kuficha sukari na vyombo vya uchunguzi vinafuatilia kote nchini na yeyote atakayebainika kufanya hujuma hizo atakabiliwa na mkondo wa Sheria.
TRA Lindi Yataifisha Na Kugawa Sukari Mifuko 5,319 Kwa Wananchi
TRA Lindi Yataifisha Na Kugawa Sukari Mifuko 5,319 Kwa Wananchi
Tarehe May 8, 2016

Mamlaka ya Mapato (TRA), Mkoa wa Lindi imetaifisha na kugawa sukari mifuko 5,319 kutoka nchini Brazil yenye thamani ya shilingi 373.5 milioni na kuigawa kwa taasisi mbalimbali kama ilivyoagizwa na Rais, Dkt. John Magufuli hivi karibuni.
Sukari hiyo ilikamatwa mwezi Februari, mwaka huu wakati ikiwa inaindizwa nchini kimagendo kutoka nchini Brazil.
Taasisi za mkoa huo zilizogawiwa sukari hiyo ni pamoja na magereza, shule maalum, kambi za wazee, shule za kawaida na hospitali.
Hivi karibuni Rais Magufuli alitoa onyo kwa wafanyabiashara wanaoficha sukari ilhali kukiwa na uhaba mkubwa wa sukari kwa wananchi hali iliyopelekea bidhaa hiyo kupanda bei kwa kasi ya ajabu na kuwafanya wananchi wengi wa hali ya chini kushindwa kumudu bei hizo.
Rais Magufuli mbali na kutoa onyo hilo kwa wafanyabiashara hao, ameagiza sukari yoyote itakayopatikana imefichwa au kuendeshwa kimagendo itaifishwe na kugawiwa bure kwa wananchi.
Subscribe to:
Posts (Atom)





















