Sunday, 14 May 2017
Trump atakiwa kusalimisha kanda za mazungumzo na James Comey
Donald Trump ametakiwa kusalimisha kanda za mazungumzo yaliorekodiwa kati yake na aliyekuwa mkuu wa FBI James Comey
Wabunge wandamizi nchini Marekani wamemtaka rais Donald Trump kusalimisha mazungumzo yoyote yaliorekodiwa kati yake na aliyekuwa mkurugenzi wa shirika la FBI James Comey aliyemfuta kazi.
Kiongozi wa Democrats katika bunge la seneti Charles Schumer alionya kuwa uharibifu wa kanda hizo utakuwa uvunjaji wa sheria.
Naye Seneta wa Republican Lindset Graham alisema kuwa Ikulu ya Whitehouse inahitaji kuwa wazi kuhusu iwapo kulikuwa na kanda zozote za rekodi za mazungumzo hayo au la.
Matamshi hayo yanajiri baada ya bwana Trump kusema katika mtandao wake wa Twitter matamshi yanayoonekana kuwa vitisho kwa mkuu huyo wa zamani wa FBI.
Alimuonya Comey wiki iliopita dhidi ya kuzungumza na vyombo vya habari akisema natumai hakuna rekodi za mazungumzo yetu.
Ikulu ya Whitehouse haijathibitisha wala kukana kuwepo kwa kanda hizo.
Bwana Schumer pia alionya kwamba masenata wa chama cha Democrats watakataa kumuunga mkurugenzi mpya wa FBI hadi pale mtaalam atakapochaguliwa kuchunguza hatua ya Urusi kuingilia maswala ya Marekani katika uchaguzi uliopita.
FBI inachunguza madai hayo pamoja na ushirikiano wa Urusi na kampeni ya rais Trump.
Rais Trump amekana uhusiano wowote na anasema bwana Comey amemhakikishia kwamba hachunguzwi.
Anasema kuwa alimpiga kalamu bwana Comey kwa sababu alikuwa ameshindwa kufanya kazi vizuri.
Wanachama wa Democrats wameshutumu Trump kwa kumfuta kazi Comey ili kujaribu kusitisha uchunguzi wa FBI.
Wafungwa 12 wapigwa risasi Papua New Guinea
Mwaka 2016 inadaiwa kuwa wafungwa walivamia lango kuu la gereza hilo
Maafisa wa magereza nchini Papua New Guinea, wamewapiga risasi na kuwauwa wafungwa 17, ambao walivunja gereza na kutoroka siku ya Ijumaa.
Polisi wamewatia mbaroni wafungwa watatu, huku wakiendelea kuwasaka wengine 50 ambao bado hawajulikani waliko tangu kutokea kwa kisa hicho katika gereza la Buimo katika mji wa Lae.
Polisi wanasema kuwa, wengi wa wafungwa waliotoroka walikuwa wahalifu sugu.
Idara ya usalama nchini humo imewatahadharisha raia kuwa macho na watoe taarifa kwa vyombo vya usalama pindi wakiwaona wafungwa hao.
Gereza hilo la Buimo huwa na msongamano mkubwa wa wafungwa na uchafu na mwaka jana wafungwa 12 waliuawa baada ya kujaribu kutoroka.
Subscribe to:
Posts (Atom)


