SAKATA LA ESCROW: WALIOGAWANA FEDHA ZA UMMA KUJULIKANA WIKI HII
Sakata la wizi wa mabilioni ya fedha za umma katika akaunti ya Escrow watuhumiwa wote kujulikana wiki hii siku ya jumatano na Alhamisi. Katika siku hizo Bunge la Jamhuri ya muungano wa Tanzania linatarajia kujadili ripoti ya escrow.
Hivi sasa Wabunge wa kila vyama wamekuwa wakikutana kuweka misimamo yao kuhusu namna watakavyoshiriki kujadili ripoti hiyo ili kuokoa mabilioni ya fedha za wananchi zilizoibwa na watendaji wa serikalini na hatimaye kugawana.
Aidha, katika Kikao cha Kamati ya Uongozi wa Bunge kilichofanyika jana asubuhi kilikubaliana suala hilo la escrow lijadiliwe kwa siku mbili badala ya moja kama iliyokuwa imepangwa awali.
Kwa upande mwingine kambi Rasmi ya Upinzan Bungeni, imeibuka na madai kwamba vigogo wanaotuhumiwa kugawana fedha za Escrow wamenyofoa baadhi ya karatasi zenye majina yao ili kuficha ushaidi ambapo wameandaa propaganda ya kuwahadaa wananchi kuwa ripoti hiyo haijakamilika.
Naye Waziri Kivuli wa Fedha, James Mbatia ametaja kurasa zilizonyofolewa katika ripoti hiyo kuwa ni zilizobeba mambo ya msingi ambazo ni ukurasa wa 57, 58 na 59.
Watanzania wanausubiri kwa hamu kubwa mjadala huo utakaorindima wiki hii ili kuwafahamu walioiba fedha za umma na kugawana huku mambo ya msingi kama ujenzi wa shule, madawa hospitalini yakikwama kutokana na tamaa ya watu wachache wasio wazalendo.