Mgogoro wa Kiuchumi Ugiriki wafikia pabaya
Ugiriki imeshindwa kutekeleza muda
uliowekwa kulipa deni la Shirika la Fedha Duniani, IMF la euro bilioni
1.6, saa chache baada ya mawaziri wa umoja wa nchi za Ulaya zinazotumia
sarafu ya euro kukataa kuongeza muda wa kulipa deni hilo ili kunusuru
uchumi wa Ugiriki.
Ugiriki ni nchi ya kwanza iliyoendelea kushindwa mkopo wa IMF katika
muda uliopangwa na sasa ni rasmi inakabiliwa na malimbikizo ya deni
hilo.Kuna wasiwasi kwamba hali hii itaiweka Ugiriki katika hatari ya kuondoka katika umoja wa nchi za Ulaya zinazotumia sarafu ya euro.
IMF imethibitisha kwamba Ugiriki imeshindwa kulipa deni lake muda mfupi baada ya kumalizika kwa muda uliokuwa umepangwa jana, Jumanne.
“Tumeiarifu Bodi ya Wakurugenzi kwamba Ugiriki kwa sasa iko katika malimbikizo ya deni na itaweza kupata fedha kutoka IMF, mara itakapolipa malimbikizo, amesema msemaji wa IMF Gerry Rice.
Kwa kumalizika kwa muda wa kulipa deni la umoja wa nchi za euro, Ugiriki haitapata mabilioni ya fedha za euro na imeshindwa kutekeleza muda uliopangwa kulipa deni la IMF.