TCRA yapiga marufuku vipindi vya ‘live’ uchaguzi mkuu 2015
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Mamlaka hiyo imebainisha kuwa kuanzia tarehe 10 Septemba 2015, na katika kipindi chote cha kampeni za uchaguzi mkuu 2015, watu ambao sio wagombea wa udiwani, ubunge, urais, wasemaji rasmi wa vyama au watu wasioteuliwa na vyama vya siasa kama wawakilishi hawataruhusiwa kushiriki katika vipindi vya moja kwa moja (Live Programmes) vinavyohusu shughuli za uchaguzi vitakavyorushwa na vituo vya utangazaji hapa nchini.
Taarifa hiyo imeongeza kuwa utaratibu huu unazingatia Kanuni Za Huduma Za Utangazaji (Maudhui) (Utangazaji Wa Uchaguzi Wa Vyama Vya Siasa), 2015, Kanuni ya 4 (f), (h), (i), 5(b), (d), (e) and (f).
Mamlaka hiyo imesema kuwa hatua hii inachukuliwa na Mamlaka ili kuweka utaratibu mzuri wa kufanya kampeni za uchaguzi ziwe za amani na utulivu huku ikiahidi kuchukua hatua kali dhidi kituo cha utangazaji kitakacho kwenda kinyume na utaratibu huu huo.
Hivi karibuni vimeibuka vipindi mbalimbali vinavyohusu uchaguzi mkuu hususani kwenye televisheni ambavyo wachambuzi wake wamekuwa waki egemea upande mmoja wakitumia lugha ya kuudhi, kuchafuana baina ya wagombea mbalimbali wa urais ikiwemo wagombea wenye upinzani mkubwa sana hivisasa ambao ni Edward Lowassa na Dk.John Pombe Magufuli.