Dr. Slaa ‘amlipua’ Lowassa, akijiuzulu siasa
Akizungumza na waaandishi wa Habari leo katika Hotel ya Serena jijini Dares salaam mkutano ulioanza majira ya saa nane za mchana na kumalizika saa tisa na nusu Dkt.Slaa amesema kuwa ameamua kujitokeza leo hii ili kukomesha upotoshaji na kuuweka wazi ukweli.
Amesema hana tabia ya kuyumbishwa na anasimamia anachokiamini kwa kuwa hana ugomvi na Kiongozi yeyote kwa kuwa siasa sio uadui na Siasa inapoongozwa kwa misingi ya upotoshaji, matokeo yake ni vurugu
Alianza kwa kuzungumzia kuto onekana katika mikutano na vikao vya Chadema ambapo amesema hakuwa likizo na hakuna aliyempa likizo yoyote,amesema kilichotokea ni kuwa aliamua kuachana na siasa tangu 28.7.2015 saa sita usiku baada ya kutoridhishwa na kilichokuwa kinaendelea ndani ya chama chake.
Amesema ni kweli alishiriki kumleta Lowassa CHADEMA Lakini alikuwa na misimamo yake ambayo iliwafanya wasielewane. Baada ya Lowassa kukatwa pale Dodoma, Gwajima ambaye amemtaja kuwa ni ‘mshenga’ wa Lowassa alimpigia simu kutaka kujua nini cha kufanya.
Kabla ya kuanza kuwasikiliza, msimamo wake ulikuwa ni kumtaka Lowassa kwanza atangaze kuhama chama, aweke wazi ni chama gani anaenda na ajisafishe juu ya tuhuma zake
Tangu akatwe jina, Lowassa hakutangaza kujitoa CCM na wala hakujisafisha na tuhuma zake, kitu kilimchomfanya atofautiane naye.
Aliwauliza wanachadema wenzake kuwa Lowassa anakuja kama Mtaji au Mzigo?
Suala sio urais kama watu wanavyozusha, yeye alikuwa anataka mgombea mwenye uwezo na sifa ambaye ataweza kuitoa CCM na hakuwa na tamaa ya urais kama watu wanavyosema
Tangu Gwajima awape taarifa za ujio wa Lowassa, Swali lake la Lowassa kuwa Mtaji au mzigo halikuwahi kujibiwa. Amesema alijibiwa kuwa anakuja na wabunge 50 wa CCM, wenyeviti 22 wa mikoa na wenyeviti 80 wa wilaya.
Baada ya ahadi hiyo, alitaka sasa apewe majina ya hawa watu lakini mpaka tarehe 25 july hakupewa hayo majina , Dkt Slaa amesema anapinga kuchukua makapi ya CCM kuyaita Mtaji.
Ameongeza kuwa kutokana na kutokuwa na maelewano na chama hicho aliandika barua ya kujiuzulu lakini hata hivyo amesema Profesa Safari aliichana ile barua.
Amesisitiza kuwa ukisema unataka kuiondoa CCM ni lazima ujikumbushe misingi ya CHADEMA ambayo ilikuwa ni uadilifu. Leo chadema hii ina Uadilifu gani?? amehoji Dr.Slaa.
Amemshangaa sana Lowassa kusimama mbele ya watu akijinasibu kuwa ni msafI na akitaka mwenye ushahidi aende Mahakamani suala ambalo amesema ni dhambi na kupotosha watu.
Katika mkutano huo amemtaka Lowassa atoke hadharani atangaze Richmond ni ya nani pamoja na kumtaja muhusika wa kampuni hiyo.
“Nahitimisha kwa kusema kuwa Nimestaafu siasa na sina chama lakini nina nchi, hivyo nitaendelea kuwatumikia watanzania.