BAADA YA KUFUNGIWA , MAWIO KUKIMBILIA MAHAKAMANI
Uongozi wa gazeti la MAWIO umeapa kwenda mahakamani kupinga uamuzi wa serikali kulifungia gazeti hilo kutochapishwa kwa kipindi cha miezi 24.
Uamuzi wa kulifungia gazeti hilo ulitangazwa jana na Serikali kupitia Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo ambapo sababu iliyotajwa ni gazeti hilo kukiuka maagizo ya serikali ya kutowahusisha marais wastaaf,u Mzee Mkapa na Dkt. Kikwete.
Mkurugenzi wa Kampuni ya Victoria Media Services Ltd ambaye pia ni Mhariri Mtendaji wa gazeti la MAWIO, Simon Martha Mkina, amesema kuwa uamuzi huo si wa haki na utapingwa mahakamani.
“Bodi itakutakana kujadili uamuzi huo kama jambo la dharura, lakini tunachoweza kukwambia kwa sasa, tutakwenda mahakamani,” amesema Mkina.
“Sina budi kulifungia gazeti lako, na kukutaka usitishe kuchapisha nakala ngumu au ya mtandaoni katika kipindi cha muda wa miezi ishirini na nne (24) tangu tarehe ya barua hii, kwa mamlaka niliyopewa chini ya Sheria ya Huduma za Habari Na. 12 ya mwaka 2016 kifungu cha 59,” ilisema sehemu ya taarifa ya Waziri Dkt. Mwakyembe iliyotolewa na Idara ya Habari Maelezo.
Gazeti hilo liliandika habari iliyokuwa na ujumbe wa jumla kuwa, marais hao wamelisababishia taifa hasara kubwa sana kutokana na usafirishaji wa mchanga nje ya nchi kwa kipindi cha miaka 19.