CCM ‘Yawacharukia’ Waliotajwa Ripoti Makinikia
Chama Cha Mapinduzi (CCM), kimewataka wote waliotajwa katika ripoti ya kamati ya pili iliyochunguza makontena 277 ya mchanga wa madini, kutoa ushirikiano kwa vyombo vya dola vitakavyowahoji.
Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Humphrey Polepole amesema hayo leo katika ofisi za Chama, Lumumba na kudai kuwa waliotajwa wote wanapaswa kutoa ushirikiano ili vyombo vya dola viweze kufanya kazi yake kwa haraka na ufanisi.
Amesema chama hicho chenye Serikali kinaviagiza vyombo vya dola kuwahoji waliohusika kwa haraka ili Watanzania wajue ukweli wa yaliyotokea.
Waliotajwa katika ripoti ya pili ni aliyewahi kuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), Andrew Chenge, waliokuwa mawaziri wa Nishati na Madini, William Ngeleja, Profesa Sospeter Muhongo na na Nazir Karamagi.
Aidha, amempongeza Rais John Magufuli kwa kuthubutu kudai rasilimali ambazo zimekuwa zikiibiwa na kuwataka wananchi kumuunga mkono Rais Magufuli kwa kazi anayoifanya badala ya kugawanyika.