Meya Manispaa ya Ubungo, Boniphace Jacob.
Meya wa Manispaa ya Ubungo, Boniface Jacob amesema kuwa mpango wa kuondolewa kwa bango la Mtaa wa Mchezaji wa Soka wa Ligi Kuu Nchini Uingereza, Victor Wanyama ni mpango ulioratibiwa kwa chuki za kisiasa dhidi yake.
Amesema kuwa aliyeratibu mpango huo ni Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda kwa madai kuwa anahakiki kama taratibu za kuupa jina Mtaa Wanyama zilifuatwa ama hapana.
Amedai kuwa kitendo hicho kimedhihirisha chuki kutokana na dalili za uwepo wa Meya huyo wa Chadema katika mchakato wa kuupa mtaa huo jina la Mchezaji Wanyama ambaye yupo nchini kwa Matembezi.
Meya Jacob amesema kuwa mchezaji huyo ambaye pia ni nahodha wa timu ya Taifa ya Kenya ‘Harambee Stars’ aliyekubali kushiriki kuangalia ligi ya Ndondo Cup alionesha nia ya kuwasaidia vijana wa kitanzania wenye hamasa ya kucheza soka lenye tija.
“Kitendo hicho ambacho si cha kiuungwana kinaweza kumkatisha tamaa mchezaji huyo ambaye angeweza kuwa rafiki mzuri wa Tanzania na kupata mafanikio kupitia mlango wa soka,” amesema.
Jacob amefafanua kuwa taratibu zote za kuupa mtaa huo jina zilipitiwa.
Victor Wanyama akizindua mtaa uliopewa jina lake katika Manispaa ya Ubungo.