Mamilioni Yafukuliwa Kutoka Ardhini
Tarehe October 4, 2016
Ilikuwa ni mshikemshike katika eneo la Mianzini mjini Arusha, ambako kuna mradi mkubwa wa upanuzi wa barabara ya kutoka Mianzini Mataa hadi Ilkiding’a unaoendelea.
Benki ya chini ya ardhi iliyosheheni mamilioni ya fedha, zilizoswekwa ndani ya mifuko myeusi ya plastiki na kufukiwa mchangani, imechimbuliwa na matrekta ya kutengeneza barabara jijini Arusha huku noti nyekundu zikitawanywa kila kona na kufanyika kuwa ‘Sandakalawe – Amina,’ kwa kila mpita njia ambaye angeweza kujitwalia fungu.
Watu walipigana vikumbo katika harakati za kujineemesha na fedha zilizokuwa zimetapakaa eneo hilo. Ikiwa imesheheni noti tupu, tena nyekundu na mpya, kufumuliwa kwa akaunti hiyo ya benki ya chini ya ardhi pamoja na kuwa neema kwa wapita njia na wakazi wa eneo hilo, kuligeuka pia kuwa kilio kwa mmiliki wa hazina hiyo, Christopher Akoonay maarufu kama ‘Mmbulu’ ambaye sasa amejipatia jina jingine la ‘Mabulungutu.’
Akonaay ni mkulima, lakini hasa akijishughulisha na ufugaji wa ng’ombe wa maziwa, yeye hudamka asubuhi kukamua mifugo hao na kisha kusambaza bidhaa hiyo ya maziwa katika maeneo mengi ya jiji katika kuwauzia wakazi wa Arusha.
Siku ya tukio, Akonaay alikuwa yuko kwenye shughuli zake za kuwapelekea maziwa wateja wake, ndipo watengeneza barabara walipofika eneo hilo la Mianzini na tingatinga zao na kuanza kuichimba njia hiyo ya kutoka Mianzini hadi Ilkiding’a katika kata ya Ilboru, inayotenganisha Jiji la Arusha na wilaya ya Arumeru.
Ikiwa imejengwa kwa fito na matope, nyumba ya ‘Mmbulu’ ilikuwa miongoni mwa zile zilizobomolewa na ni baada ya wamiliki wake, kugoma kuzibomoa wenyewe ili kupisha upanuzi wa barabara hiyo.
“Shauri letu tulilipeleka mahakamani kudai fidia kabla ya mradi wa barabara haujapita hapa, kuwa mara baada ya kesi yao kutupiliwa mbali na chombo hicho cha sheria, wajenzi hawakusubiri hata saa moja ipite, bali walikwenda moja kwa moja eneo hilo na kuanza kazi,” . amesema Akonaay.
Baadhi ya wakazi wa Mianzini, wakizungumzia suala hilo kwa masharti ya kutotajwa majina, walisema ni ajabu kwa Mzee Akonaay kuwa na kiasi kikubwa cha fedha na kuzifukia ardhini huku mwenyewe akiishi kwenye nyumba duni ya matope.
Lakini Akonaay ambaye kwa sasa anaitwa ‘Mabulungutu,’ anasema kuwa alikosa imani na benki maana wakati akifanya kazi serikalini miaka ya 1980, alifungua akaunti na akawa anaweka fedha zake zote benki.
Baada ya kustaafu mwaka 1994 na kuamua kushughulika na ufugaji, hakuzifuatilia tena fedha zake benki hadi mwaka 2000, ambako alipokwenda kuangalia fedha zake aliambiwa kuwa kwa sababu akaunti yake haikuguswa kwa zaidi ya miaka 10, alitakiwa aende Benki Kuu ya Tanzania (BoT) kujieleza. Hata hivyo, aliona huo ni usumbufu na kuamua kuanza kuweka fedha zake nyumbani.
Lakini hii pia ilimtokea puani baada ya mmoja wa ndugu zake kuzikwapua zote mara baada ya kuzifuma katika vitita vyenye thamani ya Sh milioni 20 na zaidi. Sasa Akonaay akaja na mkakati mpya wa kuhifadhi fedha kwa kuchimba shimo katikati ya chumba chake cha kulala, kilichokuwa upande wa barabara ya Mianzini na kuanza kuweka hazina yake humo.
Lakini tena, bahati mbaya ikiendelea kumuandama, makatapila ya wachonga barabara, yakaifukua benki yake hiyo ya ardhini na kutawanya fedha zaidi ya Sh milioni 35 zilizoishia kuokotwa na wapita njia pamoja na majirani, ambao kwa hofu hawakupenda hata kulizungumzia sakata hilo.