Tarehe August 6, 2016
Jeshi la Polisi Mkoa wa Dar es Salaam limetakiwa kuhakikisha kwamba sheria zinafuatwa na kusiwepo kitu kinachoitwa UKUTA ili wananchi waendelee na kazi zao kama kawaida.
Hayo yamesemwa na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda alipokuwa akizungumza na kikosi cha kutuliza ghasia katika kambi ya Ukonga Jijini Dar es salaam na kuwaambia askari hao wanafahamu sheria hivyo wasisubiri mtu yeyote kuja kuwakumbusha juu ya jambo hilo au maelekezo mengine kwa kuwa Amiri Jeshi ambaye ni Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ameshaagiza kinachotakiwa ni utekelezaji.
Amewataka kutosubiri maelekezo yoyote kutoka juu ili asiwepo mtu yeyote atakayelazimika kufunga duka kwa sababu ya UKUTA.
“Nyie ni matrekta hakuna UKUTA unaweza kusimama mbele yenu, mimi kama Mkuu wa Mkoa ninaamini hatutakuwa na vurugu kwenye Mkoa wetu na hatuwezi kuruhusu vurugu kwa kuwa tunajua madhara ya vurugu,’’ amesema.
Naye Kamanda wa Oparesheni Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi (SACP) Lucas Mkondya amesema jeshi hilo lipo vizuri na vijana wameandaliwa vizuri na wameandaliwa kuwa tayari siku nyingi na hakuna mtu yeyote atakayethubutu kufanya UKUTA na watakaofanya hivyo watazimwa kabla hawajafanya chochote.
Amewataka wananchi wote wa Jiji la Dar es Salaam kutojitokeza kwenye operesheni UKUTA kwa kuwa maandamano hayo siyo halali na watakaojitokeza watapata matatizo yasiyowahusu.
Operesheni UKUTA iliyotangazwa na CHADEMA inatarajiwa kutekelezwa Septemba 1, mwaka huu ambapo wamepanga kufanya maandamano na mikutano nchi nzima.
Tarehe August 5, 2016
Laudit Mavugo
Simba imekata mzizi wa fitina baada ya mshambuliaji aliyekuwa akisubiriwa kwa hamu kubwa, Laudit Mavugo kutua nchini jana usiku akitokea Burundi tayari kumalizana na Simba na kila kitu kilikwenda kimyakimya,Uongozi wa Simba umekuwa ukihaha kumnasa mshambuliaji huyo raia wa Burundi ambaye anakipiga katika kikosi cha Vital’O.
Tarehe August 5, 2016
Takribani shilingi bilioni mbili na milioni 123 zimekusanywa na Halmashauri ya Manispaa ya Ilala kutoka kwa wadaiwa sugu wa kodi mbalimbali baada ya kufikikishwa mahakamani.
Mwanasheria wa Halmashauri hiyo, Bonaventure Mwambaja ameyasema hayo katika kikao cha Baraza la Madiwani na kudai kuwa kwa mwaka wa fedha 2014/15 jumla ya wafanyabiashara 72 walipelekwa mahakamani ambapo hadi kufikia Julai 30, mwaka huu kiasi hicho cha fedha kilikuwa kimekwishakusanywa kutoka kwa wadaiwa hao sugu.
Amesema hadi mtu afikishwe mahakamani anakuwa ameshapatiwa hati ya madai (Demand Note) ambayo inamtaka mhusika kulipa kodi anayodaiwa ndani ya siku 14 hadi 30, na baada ya muda huo kupita basi sheria lazima ifuate mkondo wake.
Kodi hizo ni pamoja na kodi za majengo na mabango, kodi za huduma mbalimbali pamoja na kodi ya leseni za biashara.
Naye Mstahiki Meya wa Halmashauri hiyo, Charles Kuyeko ameshauri wananchi kutoa ushirikiano kwa watendaji pindi wanapowatembelea kuchukua kodi kwa kuwa ukusanyaji wa kodi huongeza pato la Taifa kwa kiasi kikubwa.