Cameroon imeondolewa katika kombe la dunia huko Brazil.
Hii ni baada ya kushindwa kwa mabao manne kwa moja na timu ya Croatia katika uga wa Manaus.
Cameroon hawakuwapa Croatia upinzani mgumu katika mchuano huu wa kundi A.Cameroon walimaliza mechi hiyo wakiwa wachezaji kumi baada ya mchezaji wa Barcelona Alex Song kuondolewa kwa kupewa kadi nyekundu.
Croatia sasa wana matumaini ya kuwania nafasi ya pili katika kundi hilo dhidi ya Brazil na Mexico ili kuendelea katika raundi ya pili.
Croatia wanajua kuwa mshindi katika mechi yao na El Tri, kama wanavyojulikana Mexico, ataendelea kwa michuano ya raundi ya pili ilhali Cameroon watamaliza kampeni yao dhidi ya wenyeji, Brazil.
Kikosi cha Niko Kovac kilishamiri katika mechi yao na Brazil katika mchuano wa ufunguzi hata ingawa walishindwa na hili lilionyeshwa hii leo pia walipoilemea timu ya Cameroon.
Katika dakika ya kumi na moja , Ivica Olic, mwenye umri wa miaka 34, akawa mchezaji mwenye umri mkubwa zaidi katika kikosi cha Croatia kuipatia timu yake bao kwenye kombe la dunia.
Ivan Perisic alimpa Olic pasi nzuri naye akamalizia kwa kufunga bao kwa mguu wake wa kushoto.
Perisic alizidi kuwa mwiba katika ngome ya Cameroon na akafunga bao lingine dakika tisa kabla ya muda wa mapumziko kwa kichwa.
Cameroon hawakuwa wametishia ngome ya Croatia kwa namna yoyote hadi wakati huo.
Mori na hasira zilizidi kuwapanda wachezaji wa kikosi cha Cameroon na hili likaletea Alex Song kuonyeshwa kadi nyekundu baada ya kumgonga kwa kumbo mchezaji Mario Mandzukic hata ingawa Mandzukic hakuwa na mpira wakati huo.
Dakika tatu baada ya kipindi cha pili kuanza, Croatia ilipata bao lake la tatu.
Bao hili lilisababishwa na kosa la kipa wa Cameroon, Charles Itandje, alipojaribu kuuondoa mpira nao ukamfikia Perisic.
Perisic, mwenye kasi, kutoka timu ya Wolfsburg ,Ujerumani aliipita safu ya Cameroon na kumpiga chenga Itandje na kisha akafunga bao .
Croatia ilizidi kuimiliki mechi hiyo huku Mandzukic akipata nafasi kadha za kuongeza mabao mengine.
Mshambulizi huyo wa Bayern Munich, alifunga mabao mawili katika mechi hiyo. Bao lake la kwanza alilifunga kwa kichwa nalo la pili likatokana na kosa lingine lake Itandje.
Kipa huyo wa Cameroon aliutema mpira hafifu kutoka kwa mchezaji wa Croatia, Eduardo.
Mpira huo ukaanguka miguuni mwa Mandzukic ambaye hakusita kumwadhibu Itandje kwa kufunga bao lingine.
Matokeo haya yamedhihirisha umaarufu na ukakamavu wa timu ya Croatia na wanatarajia kuendelea kufunga mabao dhidi ya wapinzani wao Mexico ambao waliwalemea waandalizi wa kombe la dunia,Brazil.02:33 Cameroon bila
shaka sasa wanakuwa timu ya tatu kuelekea nyumbani na ya kwanza kutoka Afrika kufunganya virago.