Thursday, 19 June 2014

HISPANIA NJE...


Uhispania yaiaga kombe la dunia Brazil.
Mabingwa watetezi wa kombe la dunia, Uhispania wameondolewa kutoka kwenye mchuano ya kombe la dunia mwaka 2014, huko Brazil baada ya kushindwa mabao 2-0 na timu ya Chile.
Matokeo hayo yaliiwacha mabingwa hao watetezi wakiwa wa mwisho na bila alama yote katika kundi B.

Kufuatia ushindi huu wa mabao 2-0 mikononi mwa Chile mabingwa watetezi wa kombe la dunia Uhispania sasa wamehakiki tikiti za ndege kurejea nyumbani pamoja na Australia .Chile pamoja na Uholanzi wanafuzu katika raundi ya pili.
Hii ni baada ya Uholanzi kushinda mechi yake ya pili na kuongoza kundi B ikiwa na alama 6 sawa na Chile.
Chile na Uholanzi hata hivyo zitakutana katika mechi ya kuamua yupi kati yao ataongoza kundi hilo.
Mshindi wa pili katika kundi B atachuana na bingwa katika kundi A inayojumuisha wenyeji Brazil na washindi wa pili katika kundi hilo Mexico.
Kwa upande wao Uhispania ambao sasa wamefungwa jumla ya mabao 7 watachuana na Australia katika mechi ambayo haitakuwa na umuhimu wowote .
Uhispania wanakodolea jicho safari ya kurudi nyumbani
Uholanzi waliishinda Uhispania kwa mabao 5-1, katika mechi ya kwanza, na baada ya mechi hii ya pili, Uhispania wanabakia bila ushindi wowote wakiwa wamefungwa mabao saba katika michuano miwili ya kombe la dunia mwaka 2014.
Hii ndio mara ya kwanza janga kama hili kuifanyikia timu ya Uhispania katika michuano ya soka ya kombe la dunia.
Chile walikua na nafasi mbili za kufunga mabao kabla hata mechi hiyo kuchukua dakika mbili.
Alexis Sanchez alianza mashambulizi ya Chile na kuisumbua safu ya ulinzi ya Uhispania.
Pasi yake safi ilimpata Eduardo Vargas ambaye shuti lake lilitoka nje baada ya kuguswa na mchezaji wa Uhispania.
Sergio Busquets alishindwa kuidhibiti kona iliyofwatia naye Gonzalo Jara akawa karibu na kuugonga mpira kwa kichwa ambao ulitoka nje hatua chache tu nje ya lango.
Uhispania ilikua imeishinda Chile matatu kwa moja katika michuano yao kumi ya awali, bila kushindwa.
Hata hivyo, timu hiyo ya mkufunzi Jorge Sampaoli, iliwapa wachile bao ambalo hata wahispania wenyewe wangependezwa nalo.
Sanchez na Arturo Vidal walipenya katika kiungo cha kati cha Uhispaniana kumpa pasi Charles Aranguiz katika eneo la hatari la Uhispania.
Huzuni miongoni mwa mashabiki wa Uhispania
Bao hili bila shaka linafaa kuwa bao zuri la ushirikiano baina ya wachezaji wa timu, katika michuano hii.
Alonso na Diego Costa walijaribu kushambulia ila mashambulizi yao hayakufua dafu kuiokoa hali ya kutatanisha ya La Furia Roja.
Matarajio ya mashabiki wa Uhispania yalizidi kudidimia wachezaji wa Chile walivyozidi kuwazuia vijana wa kikosi cha Vincente Del Bosque.
Kwa kiutani, wachezaji wa Chile walionekana kuiga mtindo mzuri wa pasi wa wahispania TIKI-TAKA na pia kuhakikisha wahispania hawauupati mpira.
Kosa la Xabi Alonso lilisababisha kufungwa kwa bao la pili.
Mkwaju wa Sanchez ulitemwa na Casillas na ukamrudia Aranguiz ambaye hakusita kuurudisha kimiani .
Costa angeweza kufunga bao baada ya muda wa mapumziko alipopewa pasi na Andres Iniesta na kumwacha akiwa moja kwa moja na kipa wa Chile Claudio Bravo.
Costa alishindwa kuudhibiti mpira na ukachukuliwa na Mauricio Isla.
Sergio Busquets na Sergio Ramos walifanya mashambulizi mengine lakini ulinzi wa Chile ulilidhibiti lango lao.
Chile walionekana kuchoka katika dakika za mwisho za mechi hiyo, hata hivyo waliweza kuhimili mashambulizi ya wahispania na kuisumbua safu ya ulinzi ya wahispania pia.

clouds stream