Magufuli aikacha Helkopta, sasa ni mtaa kwa mtaa
Mgombea urais wa CCM, Dk John Magufuli
amesema katika kampeni zake atatumia barabara ili apate kuzifahamu
kero za wananchi katika maeneo mengi ya nchi.
Licha ya kudai kuukacha usafiri huo
amefafanua kuwa maeneo mengine yenye ulazima wa kutumia usafiri mbadala,
anaweza kufanya hivyo
Akizungumza katika mkutano wake wa
kwanza tangu kuzinduliwa kwa kampeni za chama hicho katika Kijiji cha
Mishamo, kilichopo Kilometa 150 kutoka mkoani Katavi, Dk Magufuli
alisema amekataa kutumia helikopta katika baadhi ya sehemu atakazofanya
ziara, ili kujionea mwenyewe kero ya barabara inayowakabili Watanzania.
Akiwa katika kijiji cha Mishamo,
Magufuli pia aliwahakikishia wananchi wa maeneo hayo, ambao baadhi yao
waliokuwa wakimbizi waliotoka Burundi wakati wa machafuko ya mauaji ya
kimbari, lakini wakapewa uraia wa Tanzania, kwamba uongozi wake
utaheshimu na utawatambua kuwa wao ni Watanzania.
Kwa upande wa sekta ya umeme amesema
waziri atakayemteua wa umeme, akishindwa kupeleka umeme Mpanda, atoke
mwenyewe huku akisema atakuwa rais wa wanaChadema, wana ACT, wana CUF na
wasio na chama kwa kuwa maendeleo hayana chama.
Chama cha Mapinduzi (CCM) kimezindua
kampeni zake siku ya Jumapili ya Jumapili jijini Dar es salaam ambapo
wagombea wake wametimkia mikoani kusaka kura za wananchi pamoja na
kunadi sera zao.