Mkurugenzi Mkuu TCRA Na Bodi Yake Watumbuliwa
Tarehe April 26, 2016
Rais, Dkt. John Pombe Magufuli ameivunja Bodi ya Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) pamoja na kumsimamisha kazi Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka hiyo, Dkt. Ally Yahaya Simba kutokana na kutosimamia ipasavyo Mkataba wa utekelezaji wa mfumo wa Usimamizi wa Mawasiliano ya Simu (TTMS), na hivyo kuisababishia nchi kupoteza mapato ya takriban shilingi bilioni 400 kwa mwaka.
Kwa mujibu wa Mkurugenzi wa Mawasiliano Ikulu, Gerson Msigwa, Rais Magufuli amechukua hatua hiyo leo baada ya kufanya kikao kazi kati yake na uongozi na wataalam kutoka Wizara ya Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi, Wizara ya Fedha na Mipango na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU).
Rais Magufuli pamoja na kuchukua hatua hizo, amemuagiza Waziri wa Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi, Prof. Makame Mbarawa kumteua Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka hiyo maramoja.
Aidha, Rais Magufuli amewataka Waziri wa Mawasiliano Makame Mbarawa, Katibu Mkuu na Naibu Katibu katika Wizara hiyo kuchukua hatua maramoja ili mfumo wa ukusanyaji wa mapato ya simu kwa simu za ndani (Offnet) uanze kufanya kazi nan chi iweze kupata mapato yanayostahili kukusanywa.
“Waziri hakikisha unachukua hatua maramoja, nataka tukusanye mapato yote ya Serikali yanayostahili na sitasita kuchukua hatua dhidi ya yeyote atakayekwamisha jambo hili,” amesisitiza Rais Magufuli.
Mnamo Mchi 22, 2013, TCRA iliingia mkataba na kampuni ya SGS juu ya uwekezaji, uendeshaji na uhamishaji wa mapato ya simu ambayo kampuni hiyo ilipaswa kutekeleza vipengele vitano lakini mpaka sasa kampuni ya SGS haijaanza kutekeleza kipengele kidogo kinachohusiana na udhibiti wa mapato ya simu za ndani (Offnet), hali ambayo imesababisha Serikali kukosa mapato ya kiasi hicho cha fedha kilichotajwa.