Friday, 15 April 2016

Kampuni Ya Infosys Yaikana Vikali Lugumi Enterprises

Kampuni Ya Infosys Yaikana Vikali Lugumi Enterprises

Tarehe April 15, 2016infosys
infosys
Kampuni ya Infosys  IPS (T) Ltd, imejitokeza na kukanusha vikali taarifa zinazoendelea katika mitandao ya kijamii zikiihusisha kampuni hiyo na kampuni ya Lugumi Enterprises inayokabiliwa na tuhuma za ubadhirifu na mkataba mbovu baina yake na Jeshi la Polisi.
Naibu Meneja Mkuu wa Infosys, Sweki Donald amesema kuwa kampuni hiyo haijawahi kufanya biashara yoyote na kampuni tajwa ya Lugumi Enterprises na kusisitiza kuwa kampuni hizo mbili hazina mahusiano yoyote yale ya kibiashara.
Tangu kuibuke kwa kashfa ya mkataba tata kati ya Lugumi Enterprises na Jeshi la Polisi juu ya ufungwaji wa mashine za kutambua alama za vidole katika vituo vya polisi nchi nzima, kumekuwa na habari zinazosambaa kuwa kampuni ya Infosys ilipokea mabilioni ya shilingi kutoka kampuni ya Lugumi, jambo ambalo wanadai kuwa halina ukweli wowote na kutoa rai kwa umma kupuuza taarifa hizo za upotoshaji.
Katika mkataba huo wa mwaka 2011, Kampuni ya Lugumi Enterprises ilipewa tenda ya kufunga mashine za kuchukua alama za vidole katika vituo vya polisi 108 nchini kwa gharama ya Sh bilioni 37.
Tayari kampuni hiyo imekwishalipwa Shilingi bilioni 34 sawa na asilimia 99 ya fedha zote, huku ikiwa imefunga mashine katika vituo 14 tu katika jiji la Dar es Salaam ambavyo pia havijulikani vipo maeneo gani.

clouds stream