Panga Pangua Ya Kamati Za Bunge Yawakera Wabunge
Tarehe April 29, 2016
Spika wa Bunge, Job Ndugai amefanya mabadiliko mengine ya kamati za Bunge kwa kuwaongeza wabunge wapya na kuwahamisha wengine kwenda kwenye kamati nyingine, jambo ambalo limepingwa na baadhi ya wabunge wakidai linapunguza ufanisi.
Katika taarifa iliyotolewa na Kitengo cha Habari na Mawasiliano cha Bunge, mabadiliko hayo yamefanyika kwa mujibu wa kanuni ya 116 (3) na (5) ya Kanuni za Kudumu za Bunge za mwaka 2016, ili kuhakikisha kila mbunge anakuwa mjumbe wa kamati mojawapo ya Bunge.
Juzi, Kwa mara ya pili, Spika Ndugai aliwaongeza wabunge wanne wapya walioapishwa bungeni Aprili 19, kwenye kamati za Miundombinu; Ardhi, Maliasili na Utalii; Kilimo, Mifugo na Maji; na Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama.
Mbunge wa Kigoma Mjini, Zitto Kabwe (ACT Wazalendo), alisema mabadiliko hayo yanaonyesha namna ambavyo Spika Ndugai ‘anavyokosa umakini katika uundaji wa kamati hizo’.
Naye Mbunge wa Mwibara, Kangi Lugola (CCM) alisema mabadiliko yanayofanywa hayawezi kuleta tija katika bunge hilo, kwani watu wanashindwa kujipanga vyema kwa kuwa hawajui kesho itakuwaje.