Naibu Spika Azua Gumzo Kwa Kumuita Mbunge ‘ Bwege’
Tarehe April 29, 2016
“Na wewe Mheshimiwa Bwege, hebu kaa chini. Usionyeshe ubwege wako hapa,” alisema Dk Ackson kumzuia mbunge huyo asiendelee kuzungumza wakati wa mjadala.
Kitendo cha kutumia neno bwege kumuelezea mbunge huyo kilisababisha wapinzani wacharuke, na kuibua bungeni kesi ya mtu aliyefunguliwa mashtaka mkoani Arusha kwa kosa la kumuelezea Rais John Magufuli kuwa ni bwege.
Bila ya kuruhusiwa, mmoja wa Wabunge alifungua kipaza sauti na kusema: “Hatimaye msamiati wa bwege watua bungeni sasa kutumika rasmi. Futa lugha ya kuudhi; bwege bwege.”
Akizungumzia suala hilo Mbunge wa Moshi Vijijini (Chadema), Antony Komu alisema: “Kauli iliyotolewa na Naibu Spika inaonyesha wazi kuwa ni kiongozi anayekiuka misingi, taratibu na kanuni za Bunge. Tazama anatukana watu tu bila kujali jambo lolote, hii si sawa kabisa.”
Naye Mbunge wa Kalenga (CCM), Godfrey Mgimwa alisema Dk Tulia alighafilika wakati akitoa kauli hiyo baada ya kurushiwa maneno mara kwa mara na wabunge wa upinzani, tena bila kufuata kanuni na taratibu za kibunge.
Hivi karibuni Mkazi wa Arusha, Isaack Habakuk Emily alipandishwa kizimbani akikabiliwa na shitaka la kumuita Rais kuwa ni bwege.