Friday, 7 August 2015

KQ hoi: Inahitaji sindano ya trilioni 3 kupumua

KQ hoi: Inahitaji sindano ya trilioni 3 kupumua

Tarehe August 6, 2015
Kenya Airways (KQ), shirika la ndege la Kenya, na moja ya mashirika makubwa ya ndege barani Afrika iko hoi bin taabani.
Wiki iliyopita shirikahilo lilitangaza kupata hasara ya Shilingi za Tanzania bilioni 500, kiasi cha hasara kikubwa zaidi kwa kampuni kilichowahi kuripotiwa nchini humo.
Kufuatia taarifa hizo, sasa wataalam wa fedha wa Standard Investment Bank wametabiri kuwa kampuni ya KQ sasa inahitaji kiasi cha Shilingi Trilioni 2 za Tanzania kuweza kurudi katika hali ya kawaida ya uendeshaji.
Wiki iliyopita waziri wa Hazina wa Kenya Trotich alitangaza mpango wa serikali wa kuipa KQ Shilingi Trilioni 1 na bilioni 200 fedha ambazo zimepangwa kulisaidia shirika hilo kupunguza madeni yaliyoliemea kwa sasa.
Kutokana na hali mbaya ya shirika, inategemewa kuwa shirika hilo litalazimika kuchukuwa maamuzi magumu ya kujipanga upya, yakiwemo ya kupunguza wakubwa wake kwa kupunguza idadi ya ndege, wafanyakazi na hata safari.

Monday, 3 August 2015

Azam Bingwa Kagame Cup 2015

Azam Bingwa Kagame Cup 2015

Tarehe August 3, 2015
Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Saidy Meckysadick (wa pili kushoto) akimkabidhi la ubingwa wa soka Afrika Mashariki na Kati, Kagame baada ya kuifunga Gor Mahia ya Kenya 2-0 leo uwanja wa Taifa jijini Dares salaam.
Timu ya azam imetangazwa bingwa wa michuano ya vilabu bingwa afrika mashariki CECAFA kagame cup baada ya kuifunga Gor mahia ya kenya katika fainali na kuondoka na kitita cha dola 30,000 pamoja na kikombe katika mchezo uliochezwa mapema leo jijini Dar es Salaam huku ikiweka rekodi ya kucheza michuano yote bila kufungwa ndani ya Dakika 90.
Azam iliingia fainali baada ya kuitandika KCCA ya Uganda goli 1-0 huku Gor Mahi ya kenya ikiingia fainali baada ya kuitandika Khartoum ya Sudan magoli 3-1 katika michezo ya nusu fainali.
Nahodha wa timu ya Azam John Bocco (Aderbayor )akipokea zawadi ya dola 30,000
John Bocco (Adebayor) alikuwa wa kwanza kuipatia Azam bao la kwanza akiunganisha krosi ya Kipre Cheche katika dakika ya 16 ya mchezo katika kipindi cha kwanza baada ya safu ya ulinzi ya Gor mahia inayoongozwa na Haruna Shakava kupotena na kumpa Bocco nafasi ya kufumania Nyavu.
Katika kipindi cha kwanza Bocco na Kipre walikosa magoli katika dakika tofauti huku kwa upande wa Gor Mahia Michae Olunga na Erick Ochieng wakipata wakati mgumu baada ya beki wa Azam Paschal Wawa kuonyesha kuwamudu wachezaji wote hao wa Gor Mahia na mpaka mapumziko Azam walikuwa mbele kwa Goli moja.
Wachezaji wakimbeba kocha wa Timu Stewart Halll mara baada ya Timu hiyo kutangwa mabingwa.
Katika kipindi cha pili Aucho Khalid wa Gor Mahia alionekana kuichezesha timu hiyo huku akitoa pasi nyingi za pembeni zilizokuwa zikimkuta Erick Ochieng lakini jitihada zake azikuzaa matunda na Aucho Khalid alimchezea madhambi Kipre Cheche katika eneo la hatari madhambi yalioyozaa goli katika dakika ya 64 ya mchezo katika kipindi cha pili.
Mpaka dakika ya 90 Azam waliibuka washindi wa Michuano hiyo wakiwachapa Gor Mahia ya Kenya Magoli 2-0 katika mchezo wa fainali.

Sunday, 2 August 2015

Mawaziri watano Waanguka kura za maoni CCM

Mawaziri watano Waanguka kura za maoni CCM

Tarehe August 3, 2015
Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mathias Chikawe.
Matokeo ya awali kura za maoni CCM yameonekana kuwa mwiba kwa mawaziri watano pamoja na baadhi wa wabunge kupitia chama hicho kufuatia kuangushwa  na kuchaguliwa wengine.
Mawaziri walio anguka ni  Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mathias Chikawe. Ambapo alipata kura  5,128 dhidi ya Hassan Masalla, Mkuu wa Wilaya ya Kilombero aliyepata kura 6,444.
Aliyepata kuwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Utawala Bora na pia Waziri wa Katiba na Sheria akikwama katika mchakato wa kurejea bungeni, naibu wake katika Wizara wa Mambo ya Ndani, Pereira Silima naye ameanguka katika kura za maoni huko jimbo la Bumbwini, Unguja.
Mwanasiasa mwingine aliyekwama katika kura za maoni ni Mahadhi Juma Mahadhi ambaye ni Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa  katika Jimbo la Paje, Unguja huku mshindi akiibuka kuwa Jaffar Sanya Jussa.
Naibu Waziri wa Fedha, Adam Malima naye  ameripotiwa kuanguka katika kura za maoni katija Jimbo la Mkuranga mkoani Pwani.
Mwingine ni  Naibu Waziri wa Kazi na Ajira, Dk Milton Makongoro Mahanga ambaye  baada ya kuanguka ametimkia Chadema.
Kutoka  Jimbo la Mvomero mkoani Morogoro, aliyewahi kuwa mbunge wa zamani wa jimbo hilo, Suleiman Saddiq `Murad’ amefanikiwa kumwangusha mshindani wake wa siku nyingi, Amos Makalla ambaye alilitwaa jimbo hilo mwaka 2010.
Nalo Jimbo la Uzini ambako mwanasiasa nguli aliyepata kuwa waziri katika wizara mbalimbali za Serikali ya Muungano, Muhammed Seif Khatib ameshindwa katika kura za maoni.
Kwa upande wa  wabunge nao  wamekuwa na wakati mgumu majimboni kwao, akiwemo Ismail Aden Rage wa Tabora. Mbunge mwingine aliyeshindwa katika kura za maoni ni Mtutura Abdalla wa Tunduru Kusini.

clouds stream