Friday, 6 November 2015

Magufuli aanza kwa kuwashitukiza Wizara ya Fedha

Magufuli aanza kwa kuwashitukiza Wizara ya Fedha

Tarehe November 6, 2015
Rais Dkt.Magufuli akiwa Wizara ya fedha kukagua utendaji kazi wa watumishi wa wizara hiyo.
Rais Dkt.Magufuli akisaini kitabu cha wageni Wizara ya Fedha jijini Dares salaam leo.
Rais Dkt.John Pombe Magufuli leo ameanza kazi kwa kuwashitukiza watendaji wa wizara ya fedha.Aidha, Magufuli ametembea kwa miguu kutoka Ikulu jijini Dar es salaam hadi wizara ya Fedha akiwa ameongozana na maofisa wa usalama ambapo mara baada ya kufika katika ofisi ya Wizara ya Fedha aliwakuta maofisa wengine wakiwa nje ya ofisi zao.
Inadaiwa huenda akatembelea wizara nyingine za serikali yake kujionea utendaji kazi wa wafanya kazi katika serikali yake mpya ya awamu ya tano.

JK awasamehe wafungwa 4,160 akiaga Ikulu

JK awasamehe wafungwa 4,160 akiaga Ikulu

Tarehe November 6, 2015
Rais mstaafu wa awamu wa nne Dkt.Jakaya Kikwete.
Wafungwa 4,160 wamepata msamaha kutoka kwa aliyekuwa Rais wa awamu ya nne Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete aliyekabidhi nchi kwa rais mpya Dkt.John Pombe Magufuli aliyeapishwa jana jijini Dar es salaam.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mathias Chikawe kwa vyombo vya habari jana Dar es Salaam imebainisha kuwa  kati ya wafungwa hao, wafungwa 867 wataachiwa huru na wafungwa 3,293 watapunguziwa vifungo vyao na kubaki gerezani wakitumikia sehemu ya vifungo vyao vilivyobaki.
Amewataja walionufaika na msamaha huo kuwa ni wafungwa wote wapunguziwe moja ya sita ya vifungo vyao zaidi ya punguzo la kawaida linalotolewa chini ya Kifungu cha 49(1) cha Sheria ya Magereza Sura ya 58 isipokuwa wafungwa walioorodheshwa katika ibara ya 1 (i-xix).
Wafungwa  wengine kuwa ni wafungwa wagonjwa wenye magonjwa kama Ukimwi, kifua kikuu, saratani ambao wako kwenye hatua ya mwisho ambao watathibitishwa na waganga chini ya Mganga mkuu wa mkoa au wilaya.
Ameongeza kuwa  wazee wenye umri zaidi ya miaka 70, wafungwa wa kike walioingia na mimba gerezani na walioingia na watoto wanaonyonya na wasionyonya na walemavu wa mwili na akili na ulemavu huo uthibitishwe na jopo la waganga.
Katika hatua nyingine taarifa hiyo imesema kuwa msamaha hautawahusu wafungwa wenye adhabu za kunyongwa, waliohukumiwa kunyongwa na adhabu hiyo baadaye kubadilishwa kuwa kifungo cha maishaau kifungo gerezani.
Wengine ni wafungwa waliotumikia kifungo kwa makosa ya usafirishaji na utumiaji wa dawa za kulevya, makosa yanayohusu uombaji, upokeaji na utoaji rushwa, unyang’anyi na kujaribu kutenda makosa hayo, kubaka, kulawiti au kujaribu kutenda makosa hayo. Aidha, makosa mengine ambayo vifungo vyake haviko kwenye msamaha huo ni makosa ya kuwapa mimba wanafunzi, wizi wa magari, pikipiki au kujaribu kutenda makosa hayo, matumizi mabaya ya madaraka, waliowahi kupunguziwa vifungo na Rais.
Wafungwa wengine  ni  wanaotumikia vifungo kwa makosa ya wizi na ubadhirifu wa fedha za Serikali, kutoroka au kujaribu kutoroka wakiwa chini ya ulinzi halali na wafungwa wanaotumikia vifungo chini ya Sheria ya Bodi ya Parole Sheria Namba 25 ya Mwaka 1994 ya Sheria ya Huduma kwa Jamii Namba 6 ya Mwaka 2002.

Thursday, 5 November 2015

Rais Magufuli awataka wagombea wenzake kuweka itikadi pembeni


Rais Magufuli awataka wagombea wenzake kuweka itikadi pembeni

Tarehe November 5, 2015

John Pombe Joseph Magufuli (56) akiapishwa kuwa Rais wa tano wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika uwanja wa Uhuru jijini Dar es Salaam.
Sherehe za kumuapisha Magufuli zilihudhuriwa na viongozi wa ndani na nje ya nchi akiwemo Rais Rorbert Mugabe wa Zimbabwe,Joseph Kabila wa Congo,Paul Kagame wa Rwanda,Jacob Zuma wa Afrika Kusini na Raila Odinga wa Kenya.
Baada ya kuapishwa na Jaji Mkuu wa Tanzania Jaji Othaman Chande Rais John Magufuli alitoa neno la shukrani kwa watanzania na kuwataka washindani wake saba waliokuwa wakichuana katika uchaguzi mkuu uliofanyika Oktoba 25 mwaka huu kuweka   itikadi za vyama  pembeni na kushirikiana kwa  kufanya kazi kwa maslahi ya Taifa zima.
Amesema kuwa kwa kuwa uchaguzi umekwisha ni vema viongozi hao wakaweka itikadi,maslahi na matakwa yao binasfi kando na kuungana nae kujenga taifa imara.
“Uchaguzi umekwisha na Rais ni mimi John Magufuli sasa ni wakati wa kufanya kazi tu…na nitafanya kazi kwa nguvu zangu zote na kwa kumtanguliza Mungu mbele,”alisema Rais
Magufuli.
Ameongeza kuwa dhamana waliyopata kutoka kwa watanzania ni kubwa sana na ni jukumu la Serikali ya awamu ya tano kuhakikisha wanatekeleza ahadi zote walizotoa wakati wa
kampeni walipokuwa wakiomba ridhaa ya kuliongoza taifa.
Rais Magufuli hakusita kumshukuru Rais Mstaafu wa awamu ya tatu Benjamin Wiliam Mkapa ambaye alimteua kuwa waziri wa Ujenzi kwa kipindi chake chote cha miaka 10 wakati huo akiwa na umri wa miaka 35 tu.
Pia alimshukuru Rais Mstafu wa awamu ya nne Dkt Jakaya Mrisho Kikwete ambaye naye alimchagua kuwa waziri katika Serikali yake na baadae akiwa Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) kumpa dhamana ya kupeperusha bendera ya chama hico na kuwa Rais wa tano wa Jamhuri ya Muungano ya watu wa Tanzania. Magufuli ni nani? alihoji na kuendelea kusema..mpaka achaguliwe na kuaminiwa kuliongoza Taifa hili….nakosa maneno mazuri ya kuongea lakini leo sio sehemu ya kutoa hutuba nipo hapa kushukuru tu,amesema Rais Magufuli.

clouds stream