JK awasamehe wafungwa 4,160 akiaga Ikulu
Wafungwa 4,160 wamepata msamaha kutoka kwa aliyekuwa Rais wa awamu ya nne Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete aliyekabidhi nchi kwa rais mpya Dkt.John Pombe Magufuli aliyeapishwa jana jijini Dar es salaam.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mathias Chikawe kwa vyombo vya habari jana Dar es Salaam imebainisha kuwa kati ya wafungwa hao, wafungwa 867 wataachiwa huru na wafungwa 3,293 watapunguziwa vifungo vyao na kubaki gerezani wakitumikia sehemu ya vifungo vyao vilivyobaki.
Amewataja walionufaika na msamaha huo kuwa ni wafungwa wote wapunguziwe moja ya sita ya vifungo vyao zaidi ya punguzo la kawaida linalotolewa chini ya Kifungu cha 49(1) cha Sheria ya Magereza Sura ya 58 isipokuwa wafungwa walioorodheshwa katika ibara ya 1 (i-xix).
Wafungwa wengine kuwa ni wafungwa wagonjwa wenye magonjwa kama Ukimwi, kifua kikuu, saratani ambao wako kwenye hatua ya mwisho ambao watathibitishwa na waganga chini ya Mganga mkuu wa mkoa au wilaya.
Ameongeza kuwa wazee wenye umri zaidi ya miaka 70, wafungwa wa kike walioingia na mimba gerezani na walioingia na watoto wanaonyonya na wasionyonya na walemavu wa mwili na akili na ulemavu huo uthibitishwe na jopo la waganga.
Katika hatua nyingine taarifa hiyo imesema kuwa msamaha hautawahusu wafungwa wenye adhabu za kunyongwa, waliohukumiwa kunyongwa na adhabu hiyo baadaye kubadilishwa kuwa kifungo cha maishaau kifungo gerezani.
Wengine ni wafungwa waliotumikia kifungo kwa makosa ya usafirishaji na utumiaji wa dawa za kulevya, makosa yanayohusu uombaji, upokeaji na utoaji rushwa, unyang’anyi na kujaribu kutenda makosa hayo, kubaka, kulawiti au kujaribu kutenda makosa hayo. Aidha, makosa mengine ambayo vifungo vyake haviko kwenye msamaha huo ni makosa ya kuwapa mimba wanafunzi, wizi wa magari, pikipiki au kujaribu kutenda makosa hayo, matumizi mabaya ya madaraka, waliowahi kupunguziwa vifungo na Rais.
Wafungwa wengine ni wanaotumikia vifungo kwa makosa ya wizi na ubadhirifu wa fedha za Serikali, kutoroka au kujaribu kutoroka wakiwa chini ya ulinzi halali na wafungwa wanaotumikia vifungo chini ya Sheria ya Bodi ya Parole Sheria Namba 25 ya Mwaka 1994 ya Sheria ya Huduma kwa Jamii Namba 6 ya Mwaka 2002.