Monday, 4 July 2016

Maghembe Ashutumu Mawakala Utalii Kuendesha Mgomo Baridi Dhidi Ya VAT


Tarehe July 4, 2016tana4
Ikiwa ni siku chache tangu mawakala wa utali nchini kulalamika ongezeko la VAT katika sekta ya hiyo kumepelekea watalii kupungua, Waziri wa Maliasili na Utalii, Profesa Jumanne Maghembe ametoa onyo kwa mawakala wanaofungua akaunti nchi jirani ya Kenya kwa lengo la kukwepa kodi hiyo ya Ongezeko la Thamani (VAT).
Waziri Maghembe amesema Kenya sio sehemu ya Tanzania na kwamba Tanzania sio koloni la Kenya hivyo hizi ni kodi za Tanzania hata kama Kenya imetoa tozo la kodi katika sekta hiyo na kusema kuwa Tanzania haiwezi kupangiwa kodi kwa Maendeleo ya taifa letu.
“Kinachoonekana hapa ni kama vile kuna propaganda na mgomo baridi kutoka kwa baadhi ya mawakala wanaotaka kuihadaa dunia ili iione Tanzania kutoza kodi hiyo ya VAT ni tatizo kubwa,” amesema.
Hatahivyo amedai kuwa Serikali inaendelea kuangalia mwenendo wa sekta hiyo ya utalii kwa muda wa mwezi mmoja au miwili ili kuona hali inakwendaje na baada ya hapo itafanya tathmini ya kina na kasha taarifa maalum itatolewa kwa Umma.
Mawakala hao walikaririwa hivi karibuni wakidai kuwa watalii wengi wamesitisha safari zao kuja nchini kufanya utalii na badala yake wameamua kwenda nchini Kenya ambapo kodi ya VAT imeondolewa.

Sunday, 3 July 2016

VETA Yaja Na Jibu Wizi Wa Magari, Bodaboda


Tarehe July 3, 2016car-theft
car-theft
Katika jitihada za kukabiliana na wizi wa vyombo vya moto ikiwemo magari na pikikipiki Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA), imebuni kifaa maalum kitakachoweza kudhibiti wizi wa magari na pikipiki kwa kutumia simu.
Mwalimu wa Teknolojia ya Mawasiliano wa Veta-Kipawa Jijini Dar es Salaam, Valerian Sanga amesema kuwa kwa ushirikiano na wa Chuo hicho anayefundisha masuala ya umeme, Christian Brighton, wameweza kubuni kifaa hicho kilichowachukua miaka miwili kukamilika.
Kwa kutumia kifaa hicho, dereva atakuwa na uwezo wa kuzima pikipiki au gari kwa kutumia simu ya mkononi, ambayo namba yake itakuwa imefungwa katika chombo hicho cha usafiri.
“Wiki tatu zilizopita ndio tumekamilisha kifaa hiki na kuanza kufanya kazi, tukafunga kwenye pikipiki hii (akionesha) kupima na kuonesha watu namna ya kuweka ulinzi kwenye vifaa vyao kwa kuwa mifumo kama hii, inauzwa katika kampuni za nje lakini ni gharama sana,”alisema.
Ubunifu huo umepelekea mamlaka hiyo, kupata tuzo ya mshindi wa jumla wa Maonesho ya Kimataifa ya 40 Dar es Salaam, yanayoendelea katika viwanja vya Mwalimu Nyerere.
Sanga amesema kifaa hicho kina GPS na kinatumia mawasiliano ya simu kwa kutumia GSM, itakayo saidia kujua sehemu pikipiki au gari lilipo, lakini pia kikimwezesha mmiliki kuzima na kuwasha usafiri wake popote ulipo.

Rais Magufuli Awafariji Wafiwa Ajali Morogoro


Tarehe July 3, 201613528741_1133037056739711_2605549793821025833_n
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli amezitumia salamu za pole familia, ndugu, jamaa na marafiki wa watu 12 waliopoteza maisha kufuatia ajali mbili zilizotokea katika eneo moja la VETA Dakawa, Tarafa ya Dumila, Wilaya ya Kilosa Mkoani Morogoro.
Katika salamu zake kupitia kwa Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Dkt. Steven Kebwe, Rais Magufuli amesema amepokea kwa mshituko na masikitiko taarifa za vifo vya watu hao ambao licha ya taifa kupoteza nguvu kazi muhimu, ndugu, jamaa na marafiki wamepoteza watu waliowategemea na wapendwa wao.
Kwa mujibu wa Kaimu Mkurugenzi Mawasiliano, Ikulu, Gerson Msigwa, Rais Magufuli amemuomba Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Dkt. Steven Kebwe kufikisha salamu za pole kwa wote waliopatwa na msiba na kwamba anaungana nao katika kipindi hiki kigumu cha majonzi.
“Pia nawaombea wawe na moyo wa uvumilivu na ustahimilivu na Mwenyezi awapumzishe marehemu wote mahali pema peponi, Amina,”amesema Rais Magufuli.
Rais amewaombea pia majeruhi wote waliolazwa hospitali na wale wanaoendelea kupata matibabu wakiwa majumbani, kupona haraka ili waendelee na kazi zao za kila siku.
Ajali ya kwanza ilitokea majira ya saa 11:30 jioni ya tarehe 30 Juni, 2016 ambapo watu 5 wamefariki dunia kufuatia malori mawili, mojawapo likiwa na shehena ya mafuta kugongana na kisha kuwaka moto, na ajali ya pili ikatokea hapohapo majira ya saa 10:00 alfajiri ya tarehe 01 Julai, 2016 baada ya basi la kampuni ya Otta High Class kuligonga lori la mafuta lililokuwa likiungua moto na kusababisha vifo vya watu 7 mpaka sasa.

clouds stream