Tarehe July 3, 2016
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli amezitumia salamu za pole familia, ndugu, jamaa na marafiki wa watu 12 waliopoteza maisha kufuatia ajali mbili zilizotokea katika eneo moja la VETA Dakawa, Tarafa ya Dumila, Wilaya ya Kilosa Mkoani Morogoro.
Katika salamu zake kupitia kwa Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Dkt. Steven Kebwe, Rais Magufuli amesema amepokea kwa mshituko na masikitiko taarifa za vifo vya watu hao ambao licha ya taifa kupoteza nguvu kazi muhimu, ndugu, jamaa na marafiki wamepoteza watu waliowategemea na wapendwa wao.
Kwa mujibu wa Kaimu Mkurugenzi Mawasiliano, Ikulu, Gerson Msigwa, Rais Magufuli amemuomba Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Dkt. Steven Kebwe kufikisha salamu za pole kwa wote waliopatwa na msiba na kwamba anaungana nao katika kipindi hiki kigumu cha majonzi.
“Pia nawaombea wawe na moyo wa uvumilivu na ustahimilivu na Mwenyezi awapumzishe marehemu wote mahali pema peponi, Amina,”amesema Rais Magufuli.
Rais amewaombea pia majeruhi wote waliolazwa hospitali na wale wanaoendelea kupata matibabu wakiwa majumbani, kupona haraka ili waendelee na kazi zao za kila siku.
Ajali ya kwanza ilitokea majira ya saa 11:30 jioni ya tarehe 30 Juni, 2016 ambapo watu 5 wamefariki dunia kufuatia malori mawili, mojawapo likiwa na shehena ya mafuta kugongana na kisha kuwaka moto, na ajali ya pili ikatokea hapohapo majira ya saa 10:00 alfajiri ya tarehe 01 Julai, 2016 baada ya basi la kampuni ya Otta High Class kuligonga lori la mafuta lililokuwa likiungua moto na kusababisha vifo vya watu 7 mpaka sasa.