Sunday, 3 July 2016

VETA Yaja Na Jibu Wizi Wa Magari, Bodaboda


Tarehe July 3, 2016car-theft
car-theft
Katika jitihada za kukabiliana na wizi wa vyombo vya moto ikiwemo magari na pikikipiki Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA), imebuni kifaa maalum kitakachoweza kudhibiti wizi wa magari na pikipiki kwa kutumia simu.
Mwalimu wa Teknolojia ya Mawasiliano wa Veta-Kipawa Jijini Dar es Salaam, Valerian Sanga amesema kuwa kwa ushirikiano na wa Chuo hicho anayefundisha masuala ya umeme, Christian Brighton, wameweza kubuni kifaa hicho kilichowachukua miaka miwili kukamilika.
Kwa kutumia kifaa hicho, dereva atakuwa na uwezo wa kuzima pikipiki au gari kwa kutumia simu ya mkononi, ambayo namba yake itakuwa imefungwa katika chombo hicho cha usafiri.
“Wiki tatu zilizopita ndio tumekamilisha kifaa hiki na kuanza kufanya kazi, tukafunga kwenye pikipiki hii (akionesha) kupima na kuonesha watu namna ya kuweka ulinzi kwenye vifaa vyao kwa kuwa mifumo kama hii, inauzwa katika kampuni za nje lakini ni gharama sana,”alisema.
Ubunifu huo umepelekea mamlaka hiyo, kupata tuzo ya mshindi wa jumla wa Maonesho ya Kimataifa ya 40 Dar es Salaam, yanayoendelea katika viwanja vya Mwalimu Nyerere.
Sanga amesema kifaa hicho kina GPS na kinatumia mawasiliano ya simu kwa kutumia GSM, itakayo saidia kujua sehemu pikipiki au gari lilipo, lakini pia kikimwezesha mmiliki kuzima na kuwasha usafiri wake popote ulipo.

clouds stream