Wednesday, 28 October 2015

UKAWA wapinga matokeo ya urais ya NEC


UKAWA wapinga matokeo ya urais ya NEC

Tarehe October 28, 2015
Mgombea urais wa Ukawa Edward Lowassa.
Vyama vinavyounda Ukawa, wamekutana kujadili mwenendo waliouita usio halali wa kutangaza matokeo, wakiituhumu Tume ya Uchaguzi (NEC), CCM na Jeshi la Polisi kushirikiana kuhujumu matokeo.
Kwa mujibu wa viongozi hao  ambao ni  Freeman Mbowe, ambaye ni mwenyekiti wa Chadema, James Mbatia (mwenyekiti, NCCR Mageuzi) na Profesa Abdallah Safari, ambaye ni mjumbe wa Kamati Kuu ya Chadema wakizungumza  na waandishi wa habari jana Makumbusho jijini Dar es Salaam  wamesema  hawayatambui  matokeo  hayo  kwa  kuwa  yamechakachuliwa.
Mbowe alibainisha  kuwa kuna vijana kutoka Kenya, ambao wamewekwa hoteli mmoja Dar es Salaam ambao wanafanya kazi ya kuchakachua matokeo yanayotoka majimboni na baadaye kuyapeleka NEC.
Ameyataja  baadhi ya majimbo hayo kuwa ni Nyamagana, Rungwe, Kahama Mjini, Shinyanga Mjini, Kyela na Muleba Kusini.
“Kazi hii ya uchakachuaji matokeo inafanywa na CCM, inaratibiwa na NEC na wasimamizi wakubwa ni polisi,” alisema Mbowe.
Naye Profesa Safari alitoa mfano wa Jimbo laTandahimba ambako alisema NEC ilitangaza kuwa mgombea wa CCM, Dk John Magufuli alipata kura 49,098 na Lowassa kura 46,288 ambazo ni tofauti ya kura 280.
Lakini matokeo halisi kutoka kwa mawakala wetu yanaonyesha Lowasa alipata kura 44,537 na Dk Magufuli 44,253 ambazo ni tofauti ya kura 284,” alisema Profesa Safari.
Aliongeza kuwa  NEC ilitangaza kuwa Lowassa alipata kura 6,000 Jimbo laTunduma, wakati matokeo yao yanaonyesha alipata kura 32,442.
Akizungumzia  vijana waliokamatwa  Mbowe 191  ambao nane kati yao walifikishwa mahakamani jana kujibu mashtaka ya kufanya makosa ya kimtandao alisema kitendo hicho cha kuwanyima dhama hakistahili. Alisema kitendo cha polisi kuwakamata vijana hao waliokuwa wakijumlisha matokeo, kimevuruga mfumo wa ukusanyaji matokeo wa Chadema.
“Lakini sasa tunatumia fomu za mawakala wetu ambazo zinaonyesha (mgombea urais wa Chadema, Edward) Lowassa anaongoza kwa tofauti kubwa ya kura,” alisema Mbowe.
Alisema vijana hao wamekamatwa kwa kosa ambalo linafanywa na mjumbe wa Kamati ya Kampeni ya CCM, January Makamba ambaye Mbowe alisema amekuwa anatangaza matokeo ya uchaguzi na idadi ya majimbo bila ya kuchukuliwa hatua zozote.
Alipoulizwa kuhusu  utangazaji matokeo Makamba alisema kuwa hakuna tatizo la yeye kusema kuwa watashinda kwa asilimia fulani kwa sababu kila chama kimekuwa kikisema hivyo.
Mwenyekiti Mwenza Ukawa James Mbatia alisema “Hili ni janga la Taifa linalotengenezwa na binadamu huku wakijua athari zake.
Alisema kinachotokea ni kitendo cha Rais Jakaya Kikwete kukataa mapendekezo ya vyama vya upinzani waliomtaka abadili mambo manne kwenye katiba kabla ya uchaguzi ambayo ni pamoja na matokeo ya urais kuhojiwa mahakamani, kuruhusiwa kwa mgombea binafsi, mgombea urais ashinde kwa zaidi ya asilimia 50 na tume ya uchaguzi kuwa huru.

Prof. Jay, Sugu, Baba Levo wapeta uchaguzi mkuu

Prof. Jay, Sugu, Baba Levo wapeta uchaguzi mkuu

Tarehe October 28, 2015
Msanii wa Hip hop, Joseph Haule ‘Prof. Jay’
Mwanamuziki mkongwe nchini Tanzania, Joseph Haule ‘Prof. Jay’, amechaguliwa kuwa mbunge wa jimbo la Mikumi mkoani Morogoro, kupitia chama cha Demokrasia na Maendeleo ‘CHADEMA’.
Prof. Jay, ambaye alikuwa anawania ubunge ametangazwa rasmi kuwa mbunge mteule wa jimbo hilo baada ya kupata kura 32,259 dhidi ya mpinzani wa karibu, Jonas Nkya wa CCM aliyepata kura 30,425.
Kupitia mtandao wa kijamii mwanamuziki huyo ameweza kubainisha kura alizopata na kudai kuwa amepata ushindi huo kwa tofauti ya kura 1834 na kuzidi kuwashuru wananchi wa jimbo hilo na Mwenyezi Mungu kwa ushindi huo.
Sambamba na hilo Mbunge wa Mbeya mjini kupitia Chama Cha Demokrasia na Maendeleo ‘CHADEMA’, Joseph Mbilinyi ‘Sugu’ aliyekuwa mbunge jimbo hilo amefanikiwa kutetea jimbo lake kwa kupata kura zaidi ya elfu 67.

Naye mwanamuziki Baba Levo, ameibuka kidedea baada ya kushinda kura za udiwani, Kigoma Mjini kwa tiketi ya chama cha ACT Wazalendo, na kuwashukuru waliompigia kura.
Ameongeza kuwa japo anakuwa Diwani wa Kigoma mjini kwa miaka mitano lakini muziki hatouacha na atajitahidi pia kusaidia vijana wenye vipaji Kigoma, ili waweze kutambulika kwa sanaa wanazofanya.
Baba Levo
Hata hivyo kwa upande wa msanii wa filamu na mchekeshaji nchini, Rashid Mwinshehe ‘Kingwendu’, ameshindwa kutamba baada ya kukosa ubunge wa jimbo la Kisarawe kupitia Chama cha CUF.
Kingwendu, ambaye kura zake hazikutimia amedai kuwa awali alikuwa anaongoza kwa kupata kura nyingi lakini baada ya kura kuhesabiwa zilionekana kuwa pungufu na hivyo Suleiman Jafo, kuibuka kuwa mshindi.
“Nimejaribu na nimethubutu kwa mara ya kwanza kugombea nafasi kubwa ya Ubunge, nimeenda vizuri tu na sitachoka na wala sitaacha, najipanga tena kwa mara nyingine najua nimekosea wapi na nitajipanga upya na nitaenda kusomea siasa zaidi,”.

Magufuli aongoza hadi sasa; Raisi kujulikana kabla ya Alhamisi

Magufuli aongoza hadi sasa; Raisi kujulikana kabla ya Alhamisi

Tarehe October 28, 2015
Mgombea urais kupitia tiketi ya ya Chama cha Mapinduzi (CCM) Dkt. John Pombe Magufuli.
Ikiwa ni siku mbili baada ya kura za uchaguzi mkuu wa tarehe 25 Oktoba kuanza kuhesabiwa, mgombea wa kiti cha Urais cha Tanzania kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dkt John Pombe Magufuli yuko mbele kwa matokeo yaliyo tangazwa na Tume ya Taifa ya Uchaguza (NEC).
Huku matokeo kutoka majimbo 113 kati ya ya jumla ya 264 yakiwa yamekwishatangazwa hadi Jumanne usiku, matokeo yanaonesha kuwa Magufuli ameshajizolea jumla ya kura 2,461,771 (aslimia 57.21) huku minzani wake wa karibu, Edward Lowassa akiwa amepata jumla ya kura 1,764,785 (asilimia 41.01).
Wagombea wa vyama vingine vya upinzani wamejizolea chini ya asilimia 2 ya kura hadi sasa hivi.
Akizungumzia mwenendo wa utangazaji wa matokeo ya kura hizo za Urais, Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi, Jaji Mstaafu Damian Lubuva alifafanua kuwa matokeo mengine yatatangazwa kadri yatakavyopatikana na anategemea kuwa kati ya siku ya Jumatano na Alhamisi matokeo yote yatakuwa yamekwishakupatikana na Raisi mteule wa Jamuhuri ya Tanzania kwa miaka mitano ijayo kujulikana.

clouds stream