Magufuli aongoza hadi sasa; Raisi kujulikana kabla ya Alhamisi
Ikiwa ni siku mbili baada ya kura za uchaguzi mkuu wa tarehe 25 Oktoba kuanza kuhesabiwa, mgombea wa kiti cha Urais cha Tanzania kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dkt John Pombe Magufuli yuko mbele kwa matokeo yaliyo tangazwa na Tume ya Taifa ya Uchaguza (NEC).
Huku matokeo kutoka majimbo 113 kati ya ya jumla ya 264 yakiwa yamekwishatangazwa hadi Jumanne usiku, matokeo yanaonesha kuwa Magufuli ameshajizolea jumla ya kura 2,461,771 (aslimia 57.21) huku minzani wake wa karibu, Edward Lowassa akiwa amepata jumla ya kura 1,764,785 (asilimia 41.01).
Wagombea wa vyama vingine vya upinzani wamejizolea chini ya asilimia 2 ya kura hadi sasa hivi.
Akizungumzia mwenendo wa utangazaji wa matokeo ya kura hizo za Urais, Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi, Jaji Mstaafu Damian Lubuva alifafanua kuwa matokeo mengine yatatangazwa kadri yatakavyopatikana na anategemea kuwa kati ya siku ya Jumatano na Alhamisi matokeo yote yatakuwa yamekwishakupatikana na Raisi mteule wa Jamuhuri ya Tanzania kwa miaka mitano ijayo kujulikana.