Wednesday, 28 October 2015

UKAWA wapinga matokeo ya urais ya NEC


UKAWA wapinga matokeo ya urais ya NEC

Tarehe October 28, 2015
Mgombea urais wa Ukawa Edward Lowassa.
Vyama vinavyounda Ukawa, wamekutana kujadili mwenendo waliouita usio halali wa kutangaza matokeo, wakiituhumu Tume ya Uchaguzi (NEC), CCM na Jeshi la Polisi kushirikiana kuhujumu matokeo.
Kwa mujibu wa viongozi hao  ambao ni  Freeman Mbowe, ambaye ni mwenyekiti wa Chadema, James Mbatia (mwenyekiti, NCCR Mageuzi) na Profesa Abdallah Safari, ambaye ni mjumbe wa Kamati Kuu ya Chadema wakizungumza  na waandishi wa habari jana Makumbusho jijini Dar es Salaam  wamesema  hawayatambui  matokeo  hayo  kwa  kuwa  yamechakachuliwa.
Mbowe alibainisha  kuwa kuna vijana kutoka Kenya, ambao wamewekwa hoteli mmoja Dar es Salaam ambao wanafanya kazi ya kuchakachua matokeo yanayotoka majimboni na baadaye kuyapeleka NEC.
Ameyataja  baadhi ya majimbo hayo kuwa ni Nyamagana, Rungwe, Kahama Mjini, Shinyanga Mjini, Kyela na Muleba Kusini.
“Kazi hii ya uchakachuaji matokeo inafanywa na CCM, inaratibiwa na NEC na wasimamizi wakubwa ni polisi,” alisema Mbowe.
Naye Profesa Safari alitoa mfano wa Jimbo laTandahimba ambako alisema NEC ilitangaza kuwa mgombea wa CCM, Dk John Magufuli alipata kura 49,098 na Lowassa kura 46,288 ambazo ni tofauti ya kura 280.
Lakini matokeo halisi kutoka kwa mawakala wetu yanaonyesha Lowasa alipata kura 44,537 na Dk Magufuli 44,253 ambazo ni tofauti ya kura 284,” alisema Profesa Safari.
Aliongeza kuwa  NEC ilitangaza kuwa Lowassa alipata kura 6,000 Jimbo laTunduma, wakati matokeo yao yanaonyesha alipata kura 32,442.
Akizungumzia  vijana waliokamatwa  Mbowe 191  ambao nane kati yao walifikishwa mahakamani jana kujibu mashtaka ya kufanya makosa ya kimtandao alisema kitendo hicho cha kuwanyima dhama hakistahili. Alisema kitendo cha polisi kuwakamata vijana hao waliokuwa wakijumlisha matokeo, kimevuruga mfumo wa ukusanyaji matokeo wa Chadema.
“Lakini sasa tunatumia fomu za mawakala wetu ambazo zinaonyesha (mgombea urais wa Chadema, Edward) Lowassa anaongoza kwa tofauti kubwa ya kura,” alisema Mbowe.
Alisema vijana hao wamekamatwa kwa kosa ambalo linafanywa na mjumbe wa Kamati ya Kampeni ya CCM, January Makamba ambaye Mbowe alisema amekuwa anatangaza matokeo ya uchaguzi na idadi ya majimbo bila ya kuchukuliwa hatua zozote.
Alipoulizwa kuhusu  utangazaji matokeo Makamba alisema kuwa hakuna tatizo la yeye kusema kuwa watashinda kwa asilimia fulani kwa sababu kila chama kimekuwa kikisema hivyo.
Mwenyekiti Mwenza Ukawa James Mbatia alisema “Hili ni janga la Taifa linalotengenezwa na binadamu huku wakijua athari zake.
Alisema kinachotokea ni kitendo cha Rais Jakaya Kikwete kukataa mapendekezo ya vyama vya upinzani waliomtaka abadili mambo manne kwenye katiba kabla ya uchaguzi ambayo ni pamoja na matokeo ya urais kuhojiwa mahakamani, kuruhusiwa kwa mgombea binafsi, mgombea urais ashinde kwa zaidi ya asilimia 50 na tume ya uchaguzi kuwa huru.

clouds stream