Monday, 28 December 2015

CCM Wajipanga Uchaguzi Wa Marudio Zanzibar

CCM Wajipanga Uchaguzi Wa Marudio Zanzibar

Tarehe December 28, 2015
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduz Dk Alli Mohamed Shein.(aliyekaa) pembeni ni Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar Vuai Ali Vuai.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduz Dk Alli Mohamed Shein.(aliyekaa) pembeni ni Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar Vuai Ali Vuai.
Chama Cha Mapinduzi (CCM) Zanzibar   chini ya Mwenyekiti wake Dk Ali Mohamed Shein kimewataka wananchi na wanachama kujiandaa kwa uchaguzi mkuu wa marudio visiwani humo.
Kwa mujibu wa taarifa ya Katibu wa Itikadi na Uenezi Zanzibar, Waride Bakari Jabu, amesema wananchi wametakiwa kujiandaa kwa uchaguzi wa marudio na kuachana na propaganda zinazotolewa na watu wachache kwa lengo la kupotosha ukweli..
Amesema  matokeo ya Uchaguzi Mkuu wa Zanzibar wa Oktoba 25 ulifutwa na Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC), Jecha Salum Jecha kwa kile alichoeleza ni kuwepo kwa ukiukwaji wa kanuni na sheria za uchaguzi huru wa kidemokrasia.
Aidha, chama hicho  kimepongeza na kutoa baraka kwa mazungumzo yanayoendelea ya viongozi wakuu wa kisiasa yakiwa na lengo la kuleta amani ya kudumu. Kamati ya mazungumzo ya hali ya kisiasa Zanzibar yenye lengo la kusaka amani ya kudumu iliyovurugika kutokana na kufutwa kwa uchaguzi mkuu.
Kamati hiyo  inaundwa na viongozi wastaafu wakiwemo marais, Dk Salmin Amour, Amani Abeid Karume, Balozi Seif Ali Iddi ambaye ni Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Makamu wa Kwanza wa Rais Zanzibar, Seif Sharif Hamad na Rais wa Zanzibar, Dk Ali Mohamed Shein.
Kwa upande wake  Rais wa Zanzibar, Dk Shein baada ya kufanya mazungumzo na Rais John Magufuli alisema mazungumzo hayo yanaendelea vizuri na taarifa kamili itatolewa  yatakapofikia tamati.
Alipoulizwa kuhusu hatma ya CCM kama uchaguzi mkuu utaorudiwa, Waride alisema chama bado kiko imara na hakijatetereka.
Licha ya chama cha Mapinduzi kujiandaa na uchaguzi mkuu Zanzibar, chama cha Upinzani cha CUF bado hakijatoa tamko lolote hadi sasa kufuatia kupinga vikali kurudiwa uchaguzi mkuu  visiwani humo.

clouds stream