Ridhiwani Aukana Utajiri, Atoa Tamko Utoroshwaji Makontena
Tarehe December 26, 2015
Familia ya aliyekuwa Rais wa awamu ya nne Dkt Jakaya Kikwete kupitia Mbunge wa Chalinze, Ridhiwani Kikwete, ambaye ni mtoto wa Rais Mstaafu Jakaya Mrisho Kikwete akiiwakilisha familia ametoa kauli kuhusiana na kuhusishwa na tuhuma za upitishaji makontena bila kulipiwa kodi bandarini.
Akizungumzia sakata hilo Ridhiwani alisema baada ya Rais Kikwete kumaliza muda wa miaka 10 madarakani, baadhi ya watu wamekuwa wakiiandama familia yao kwa tuhuma mbalimbali.
Alizitaja tuhuma hizo kuwa ni utoroshaji wa makontena kwenye bandari ya Dar es Salaam na kusisitiza kwamba tuhuma zote zinazotolewa hazina ukweli wowote bali zimelenga kumchafua yeye na familia yake.
Ridhiwani alisema tangu serikali ya awamu ya tano ianze kuwabana watu wanaokwepa kulipa kodi za serikali,baadhi ya watu wanafanya jitihada za kumhusisha na watuhumiwa hao.
Alisema hajawahi kuagiza bidhaa yoyote kutoka nje,kuwa na kontena la kulipiwa ushuru,kukwepa au kumuombea msamaha wa kupunguziwa kodi mfanyabiashara yeyote aliyeagiza kontena kutoka nje, hivyo mwenye ushahidi juu ya hilo autoe.
“Kama kuna mtu mwenye ushahidi autoe hadharani mimi niuone,dunia iuone, nawahakikishia ushahidi huo haupo na hautokuwepo labda uwe wa kughushi na wakifanya hivyo wataumbuka.
Kuhusu madai ya kumiliki Malori, mabasi na vituo vya mafuta Ridhiwani amesema ,
“Sina na sijawahi kumiliki lori au basi katika maisha yangu.Sina hisa wala ubia na mtu yeyote au kampuni ya malori au mabasi.” Alisema Ridhiwani
“Naambiwa hapa nchini siku hizi kila jengo jipya linalojengwa inasemekana ni langu na vituo vipya vya mafuta naambiwa ni vyangu.Huo ni uongo mtupu”.Amesema Ridhiwani
Amesisitiza kuwa wanaosema, kuandika na kueneza maneno hayo wanajua wanasema uongo isipokuwa wanafanya hivyo kwa nia mbaya dhidi yake na familia yake.