Mtoto Wa Rais Atajwa ‘Kusuka Njama’ Za Kumng’oa Kitwanga
Tarehe May 23, 2016
Sakata la kuvuliwa Uwaziri kwa aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Ndani, Charles Kitwanga limechukua sura mpya kufuatia Madiwani wa Jimbo la Misungwi pamoja na wakereketwa kujitokeza na kuwataja waliohusika katika kusuka njama za kuhakikisha Waziri huyo anavuliwa madaraka.
Akizungumza na Waandishi wa Habari jijini Dar es salaam leo Mwakilishi wa Madiwani hao Baraka Kingamkono amesema Waziri Kitwanga hakulewa kama ambavyo imetafsiri sababu ya kumvua uongozi bali alikuwa anatafutwa ili kufanikisha lengo la kumvua madaraka.
Amesema kuondolewa kwake kumesukwa na watu wa Nida hususani waliovuliwa madaraka, Mbunge wa Chalinze Ridhiwani Kikwete, Mfanyabiashara Said Lugumi pamoja na kundi linalodaiwa kutoka NSSF pamoja na Wabunge wa CCM pamoja na wa Upinzani.
Licha ya vigogo hao pia madiwani hao wamesema kundi la wafanyabishara wa Madawa ya Kulevya lenye mtandao mpana serikalini nalo limehusika katika kupanga nguvu kubwa kuhakikisha kuwa Waziri huyo anang’olewa Madarakani.
Kingamkono amesema kilichowashangaza wao kama madiwani waliokuwepo Bungeni hapo ni kuwepo kwa kundi la watu wa NIDA, NSSF na Uhamiaji kufanya sherehe baada ya maamuzi ya Rais kutolewa, jambo lilionesha kuwa wanafurahia kuvuliwa madaraka kwa Mbunge huyo.
Katika Hatua nyingine Mwakilishi wa Madiwani hao amesema Kitwanga alikuwa Mbunge na Naibu Waziri kwa Miaka 10 hakuwahi kuonekana kazini akiwa amelewa.
Madiwani hao pia wamesema hizo ni tuhuma za kupikwa na zinalenga kumchafua Mbunge Kitwanga ambaye alikuwa anaongoza huku akiwa na maadui wengi ndani ya Serikali, CCM na Nje ya CCM pamoja na Mtandao wa Madawa ya Kulevya.