Cameroon Yapata Pigo Lingine
Tarehe May 11, 2016
Taifa la Cameroon limepata pigo lingine baada ya kipa wa timu ya Taifa ya wanawake, Jeanine Djomnang, kupoteza maisha wakati akifanya mazoezi katika timu yake ya Femina Stars Ebolowa.
Mchezaji huyo alipoteza maisha akiwa njiani wakati anakimbizwa hospitali, ambapo inadaiwa kwamba alipatwa na mshtuko wa moyo mazoezini, huku Shirikisho la Soka la Cameroon likieleza kuwa bado halijapata taarifa kutoka kwa madaktari.
Wiki moja kabla ya kifo chake, kipa huyo aliwahi kulalamika anasumbuliwa na matatizo ya kifua na kwenda hospitali ambako alipatiwa matibabu na baadaye kujiunga na timu yake.
Tukio hilo ni mshtuko mkubwa kwa Taifa la Cameroon, kwani ni siku mbili imepita tangu nyota mwingine wa timu ya taifa ya wanaume, Patrick Ekeng, kupoteza maisha nchini Romania wakati akiitumikia klabu yake ya Dinamo Bucharest katika mchezo wa ligi.
Ekeng ambaye alikuwa na umri wa miaka 26, alianguka peke yake uwanjani bila kugongana na mchezaji yeyote katika mchezo huo zikiwa zimepita dakika saba tangu aingie akitokea benchi.
Shirikisho la Soka la Cameroon, lilielezea kusikitishwa kwake na msiba huo na kudai kuwa litaungana na familia ya marehemu ambapo pia limeandaa daftari la rambirambi kwa wachezaji hao ambalo lipo katika ofisi za makao makuu jijini Yaounde.
Kabla ya msiba huo kumalizika, shirikisho hilo limetangaza tena kifo cha Jeanine ambaye amepoteza maisha akiwa na umri wa miaka 26, ambapo limeelezea kuguswa kwa kiasi kikubwa kwa kuwapoteza wachezaji hao waliokuwa wakiipeperusha vyema bendera ya taifa.
Jeanine alikuwa akitarajiwa kulisaidia Taifa lake katika michuano ya Kombe la Mataifa ya Afrika kwa Wanawake, iliyopangwa kuanza kutimua vumbi Novemba 19 hadi Desemba 3, mwaka huu ambapo Cameroon ni wenyeji wa michuano hiyo.
Vifo vya Jeanine na Ekeng vimewagusa wadau wengi na kuacha maswali mengi kuwa ni kwanini wachezaji wengi wanapoteza maisha kwa kuanguka bila ya kugongana na mchezaji mwenzake.
Nyota wa zamani wa timu ya Taifa ya Cameroon, Marc Vivien Foe, pia alipoteza maisha uwanjani wakati akiichezea timu hiyo katika mchezo dhidi ya Colombia mwaka 2003 na kuanguka dakika ya 72 akiwa peke yake katikati ya uwanja.
Ekeng ambaye alifariki dunia wiki iliyopita, naye alianguka katikati ya uwanja dakika ya 70 hali inayowafanya watu wajiulize ni kwanini matukio hayo yanatokea kwa wachezaji wa Cameroon tu.