Rais Museveni Aapishwa Rasmi Huku Rais Magufuli Akishuhudia
Tarehe May 12, 2016
Rais wa Uganda, Yoweri Kaguta Museveni ameapishwa rasmi leo kuwa Rais wa nchi hiyo katika viwanja vya Kololo na kuhudhuriwa na viongoni mbalimbali.
Miongoni mwa viongozi walioshuhudia tukio hilo la kihistoria ni Mwenyekiti wa Jumuiya ya Afrika Mashariki na Rais wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli.
Tukio hili linatokea huku aliyekuwa mpinzani mkubwa wa Rais Museveni katika uchaguzi mkuu nchini humo Dkt. Kiza Besigye akiwa mikononi mwa polisi baada ya hapo jana kuamua kujiapisha mwenyewe kama Rais wa nchi hiyo.
Besigye amekuwa akipinga ushindi wa Museveni tangu matokeo ya uchaguzi huo yalipotolewa kwa madai kuwa uchaguzi huo haukuwa huru na wa haki.
Mgombea mwingine aliyekuwa akipinga ushindi wa Museveni na hadi kufikia hatua ya kufungua kesi Mahakamani, ni aliyekuwa Waziri Mkuu wa zamani wa nchi hiyo Amama Mbabazi.
Hata hivyo Mahakama ya Juu nchini humo ilitupilia mbali kesi hiyo na kudai kuwa Museveni alishinda kihalali katika uchaguzi huo uliofanyika Februari, mwaka huu.
Kwa mujibu wa matokeo yaliyotangazwa na Tume, Museveni alipata asilimia 60.7 ya kura zote, huku Dkt Besigye akiambulia asilimia 35.4 na Mbabazi asilimia 1 ya kura zote.