Nape Amtaja Aliyezuia Bunge ‘Live’
Tarehe May 15, 2016
Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Nape Nnauye amesema kwamba kuanzishwa kwa studio inayoratibu matangazo ya vikao vya Bunge, vinavyoendelea mjini Dodoma, ni uamuzi uliopitishwa na wabunge wenyewe na hauna mkono wa Serikali, kama inavyodhaniwa na watu wengi.
Nape alisema hayo wakati akihitimisha mjadala wa bajeti ya wizara yake kwa mwaka wa fedha 2016/2017, ambapo jumla ya Sh bilioni 20.33 zilipitishwa.
“Uamuzi wa kuanzisha studio ya Bunge si wa Nape wala Serikali, ulipitishwa na Bunge wakati Nape wala Serikali ya Awamu ya Tano, haijaingia madarakani, walipitisha na bajeti, Kanuni ndo zikasema chombo cha utangazaji kitatangaza mikutano ya Bunge kwa utaratibu na mipango ya Bunge, sasa kuingizwa Serikali kunatoka wapi?” Alihoji.
Alisema Serikali kama wasimamizi wa habari, wapo tayari kusimama kati ya Bunge na wadau wa habari, kuzungumzia upungufu uliopo, ili kupatia ufumbuzi kuhusu studio hiyo na kutorushwa kwa vikao vya Bunge moja kwa moja kama ilivyokuwa zamani.
“Mlikaa wenyewe wabunge mkapanga kuanzishwa kwa studio hii na taratibu zake sio sisi Serikali, tafadhali twendeni taratibu, tusibebeshane mzigo,” alisema.
Aliwataka wabunge kutenda haki na kuacha kusema Tanzania hakuna uhuru wa habari, wakati ripoti ya Shirika la Waandishi wa Habari Wasio na Mipaka, imeonesha katika nchi 180, Tanzania ni ya 11 yenye uhuru wa habari na kwa Afrika Mashariki ni ya kwanza kwa uhuru wa habari.
Alisema katika Muswada wa Sheria ya Huduma za Habari, wameweka haki zote za wanahabari na utaeleza elimu anayopaswa kuwa nayo mwanahabari ili kuondokana na ‘makanjanja’. Mchakato wa utungaji wa sheria hiyo utakamilika hivi karibuni, hivyo kuanza kutumika.