TRL: Mabehewa 22 yaliyoagizwa kutoka Korea Kusini ni mapya ?
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa leo na ofisi ya ofisa uhusiano wa shirika hilo imesema kwamba mabehewa hayo yalifanyiwa majaribio na TRL na kuridhika kuwa hayana kasoro yoyote.
Mabehewa hayo yaliwasili nchini Desemba,2014 ambapo shirika hilo lilipeleka maombi katika Mamlaka ya Udhibiti wa Usafrishaji wa Nchi kavu na Majini (SUMATRA) kwa lengo la kuruhusiwa kuanzisha huduma ya treni ya abiria ya Deluxe ambapo pia nauli maalumu itatozwa kwa abiria hao.
Taarifa hiyo imeongeza kuwa mabehewa yote yapo ndani ya mkataba ambao umewekwa masharti maalumu ikiwemo masharti ya gharama kwa mtengenezaji kuyafanayia marekebisho endapo hitilafu zitajitokeza wakati wa kipindi cha majaribio.
Mikataba imetoa dhamana ya kati ya mwaka mmoja na miwili kwa ajili kurekebisha hitilafu zozote zitakazojitokeza wakati wa matumizi.
Katika hatua nyingine mabehewa yanatarajiwa kutumiwa katika huduma mpya iliyopewa jina la Deluxe kwenda mkoani Kigoma kuanzia April 1, 2015.