Yanga noma, yawachakaza wazimbabwe bila huruma
Yanga wameendeleza ubabe kwa kuutumia vyema uwanja wa nyumbani kwa kuitandika FC Platinum kwa goli 5-1 kwenye mchezo wa raundi ya kwanza ya kombe la shirikisho barani Afrika mchezo uliopigwa leo jioni kwenye uwanja wa Taifa jijini Da es Salaam.
Salum Telela alianza kuifungia Yanga goli la kwanza dakika ya 26 kabla ya Haruna Niyonzima kuongeza bao la pili dakika ya 40 baada ya Amis Tambwe kutandika shuti kali lililotemwa na kipa wa FC Platinum na kumkuta Mnyaruanda huyo aliyeukwamisha mpira wavuni, lakini dakika ya 45 Walter Musona akaipatia FC Platinum goli la kufutia machozi kwa mpira wa adhabu ndogo uliomshinda golikipa wa Yanga Ally Mustafa ‘Bathez’.
Kipindi cha pili kilianza kwa kasi kubwa huku Yanga wakiliandama lango la wapinzani wao kwa muda mwingi kitu kilicho wachanganya FC Platinum. Dakika ya 46 Amis Tambwe akaifungia Yanga goli la tatu akiunganisha krosi safi iliyochongwa na Mrisho Ngassa, goli hilo liliwaamsha Yanga na kuona wanaweza kupata magoli mengi zaidi.
Mrisho Ngassa aliyekuwa msumbufu na mwiba mkali kwenye safu ya ulinzi ya wazimbabwe alifunga goli la nne mnamo dakika ya 52, lakini hakuishia hapo kwani dakika ya 90 alifunga goli lake la pili na la tano kwa upande wa Yanga akimalizia pasi ya Mliberia Kpah Sherman.
Mchezo wa marudio utachezwa jijini Harare, Zimbabwe majuma mawili yajayo, Yanga wanatakiwa kutoridhika na ushindi wao na kubweteka kwani lolote laweza tokea kwenye soka. Mfano mzuri ni wao wenyewe walivyokumbana na upinzani mkali kwenye mechi yao ya marudiano kwenye hatua ya awali dhii ya BDF XI ya Botswana.
Lakini pia Azam wakiwa Sudan walishindwa kutamba na kuzuia kufungwa goli 3-0 mbele ya Al- Merreikh na kutupwa nje ya mashindano, wanachotakiwa ni kuwa na nidhamu ya mchezo na kujiandaa kushinda mechi yao ya pili ili kusonga mbele.