Sunday, 1 March 2015

Homa ya pambano la watani wa jadi yaanza kupamba moto

Homa ya pambano la watani wa jadi yaanza kupamba moto


Maandalizi kwa ajili ya pambano la watani wa jadi tayari yameanza kushika kasi kutokana na timu zote mbili za Simba na Yanga kuingia kambini kujiweka tayari kwa ajili ya pambano hilio linalo tarajiwa kupigwa siku ya Jumapili, Machi 8 mwaka huu kwenye uwanja wa Taifa.
Timu ya Yanga SC imetua Dar es salaam jana majira ya saa 2:00 usiku ikitokea Gaborone, Botswana na moja kwa moja ikaelekea mjini Bagamoyo kuweka kambi kwa ajili ya kujiandaa na mechi dhidi ya JKT Ruvu na mechi ya Jumapili dhidi ya Simba SC.
Simba wao jana walielekea visiwani Zanzibar kwa ajili ya kuweka kambi kujiandaa na mechi ya dhidi ya watani wao wa jadi.
Simba wataingia katika mechi ya Jumapili wakiwa na kumbukumbu ya ushindi mnono wa magoli 5-0 waliouvuna Jumamosi iliopita uwanja wa Taifa dhidi ya timu vibonge, Tanzania Prisons.
Mikakati kwa ajili ya  mechi ya Jumapili imeanza kwatimu zote mbili. Kama inavyojulikana, Simba na Yanga ni mechi yenye mambo mengi, vituko, fitina, mizengwe, lengo ni kwa kila mmoja kuibuka na ushindi.
Mechi ya aina hii inawaletea shida watu wengi, wachezaji, makocha na viongozi, hata mashabiki pia ambao huzimia uwanjani na kupata taabu nyingi kwasababu ya mapenzi yao juu ya timu hizi.
Simba na Yanga wamekuwa katika nafasi tofauti. Wanajangwani wana pointi 31 kileleni, Simba wapo nafasi ya nne kwa pointi 23. Tofauti ya pointi ni 8.
Msimu huu Yanga wamekuwa na mafanikio ya uwanjani kuliko Simba, lakini hicho si kigezo cha kusema Yanga watashinda kirahisi siku ya Jumapili.
Simba mbovu alishawahi kuibania Yanga bora, na Yanga mbovu ilishawahi kuibania Simba bora mara nyingi tu. Mechi za Simba na Yanga si za kuweka rehani vitu vyako.
Maandalizi ya mechi hii ni ya aina yake, watu kuwekewa ulinzi mkali kambini ni jambo la kawaida, wachezaji kupokonywa Simu ni kawaida, watu kutoingia vyumbani kawaida tu, yote haya yanafanyika kwasababu ushindi una thamani kubwa katika mechi hii.
Simba wanasikika wakisema hata tufungwe na Kagera Sugar,Mbeya City, Stand United, lakini kwa Yanga hatukubali. Sasa wamekimbilia visiwani Zanzibar.
Yanga wanachagizwa na ushindi wa 3-0 dhidi ya Prisons, 3-1 dhidi ya Mbeya City, halafu wamewaondosha BDF XI kwenye kombe la shirikisho barani Afrika.
Kocha na viongozi wa Simba wanadai wanaijenga timu. Siku za hihi karibuni kocha mkuu wa Simba Goran Kopunovic alisikika akisema, kikosi chake ni kichanga mno, kinahitaji muda, hahitaji miaka 10, lakini anahitaji muda wa kuijenga timu.
Kwa upande wa Yanga, kocha mkuu na viongozi, wanaamini wana timu ya ubingwa. Hakuna wachezaji wa kujifunza, asilimia kubwa ya wachezaji wa kikosi cha kwanza ni wale watu wa kazi, muda wa kujifunza ulishapita, sasa wanacheza mpira.
Lakini kwenye mechi ya ‘Nani Mtani Jembe’ mwezi Desemba mwaka jana Simba iliishinda Yanga kwa goli 2-0. Ni vijana hawahawa wa Simba ndiyo walioiadhibu Yanga iliyosheheni nyota wenye uzoefu.

clouds stream