Mfalme aingilia kati ghasia za wageni kutimuliwa Afrika Kusini
Mfalme wa Jamii wa Wazulu nchini Afrika Kusini, Goodwill Zwelithini, anatarajiwa kutoa wito kwa raia wa nchi hiyo kujiepusha na ghasia, kufuatia kuongezeka kwa mashambulio ya kibaguzi nchini humo.
Mfalme huyo ameshutumiwa kwa kuchochea mashambulio hayo ambayo yamesababisha vifo vya watu saba, alinukuliwa akisema kuwa raia wote wa kigeni wanapaswa kurejea katika mataifa yao.
Maelfu ya watu wanatarajiwa kufurika uwanja mmoja ulioko mji wa Mashariki wa Durban kusikiliza hotuba hiyo ya Mfalme Zwelithini.
Kwa upande wake Rais wa nchi hiyo Jacob Zuma, amesema mashambulio hayo yanakwenda kinyume na maadili yote wanayoamini.
Makundi kadhaa yaliyojihami yameshambulia na kupora maduka kadhaa yanayomilikiwa na wahamiaji kutoka mataifa mengine ya Afrika.